Lionesses na Simbas wasalia katika nafasi zao viwango vya raga
Na GEOFFREY ANENE
TIMU za raga za Kenya za wachezaji 15 kila upande za Lionesses (wanawake) na wanaume (Simbas) zimekwamilia katika nafasi za 28 na 32 kwenye viwango bora vya dunia vilivyotangazwa Ijumaa.
Lionesses ililipua Makis ya Madagascar 35-5 Agosti 9 katika mechi ya ufunguzi ya mchujo wa kuingia Kombe la Dunia mwaka 2021 unoendelea jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini. Warembo wa kocha Felix Oloo watarejea uwanjani kuvaana na mahasimu wa tangu jadi Uganda hapo Agosti 13.
Madagascar, ambao hawakuwa wameorodheshwa katika viwango hivi, walinufaika pakubwa kucheza na Kenya. Wanavisiwa hao wameingia katika viwango hivi vya mataifa 55 katika nafasi ya 41.
Kuimarika kwao kumesukuma chini mataifa 14 ikiwemo Uganda, ambayo imeshuka kutoka 44 hadi nambari 45 baada ya kufundishwa jinsi ya kusakata raga ilipoaibishwa 89-5 na Afrika Kusini katika mechi ya kutafuta tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia.
Afrika Kusini inasalia nambari moja barani Afrika katika nafasi ya 11 duniani. Inafuatiwa na Kenya (28 duniani), Zambia (35), Namibia (39), Madagascar (41), Zimbabwe (42) na Uganda (45) katika usanjari huo.
New Zealand inaongoza viwango vya wanawake pamoja na vile vya wanaume duniani. Katika viwango vya wanaume, Wales ni nambari mbili ikifuatiwa na Jamhuri ya Ireland na Uingereza iliyoruka Afrika Kusini na kuisukuma katika nafasi ya tano.
Uingereza iliimarika baada ya kupepeta Wales 33-19. Wales ingeng’oa New Zealand kileleni kama ingelima Uingereza. Namibia ni ya kwanza barani Afrika baada ya Afrika Kusini katika nafasi ya 23 duniani.
Simbas ya Kenya inashikilia nafasi ya 32 baada ya kulemewa 30-29 katika mechi yake ya shindano la Victoria Cup mnamo Agosti 3 mjini Bulawayo. Vijana wa kocha Paul Odera wanatarajiwa kualika nambari 65 duniani Zambia katika mechi yao ijayo ya Victoria Cup mnamo Agosti 17 jijini Nairobi.