Michezo

Lionesses na Simbas zapanda viwango vya raga

July 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

TIMU za wanawake (Lionesses) na wanaume (Simbas) za raga ya wachezaji 15 kila upande za Kenya zimeimarisha pointi zao kwenye viwango bora vya dunia baada ya kushinda Uganda na kuhifadhi mataji ya mashindano ya Elgon Cup jijini Kampala mnamo Julai 13, 2019.

Lionesses ilibwaga Uganda 35-5 katika mechi ya marudiano na kuruka Guyana, Romania na Norway. Imetulia katika nafasi yake bora duniani ya 28 baada ya kujiongezea alama 1.14.

Warembo wa kocha Felix Oloo, ambao walikuwa wamepepeta Waganda hao 44-14 katika mechi ya mkondo wa kwanza mjini Kisumu mnamo Juni 22, sasa wana jumla ya alama 45.84. Uganda ina alama 38.16. Imeteremka nafasi tatu hadi nambari 44 duniani.

Mabadiliko mengine kwenye viwango vya wanawake ni Ufaransa kurukia nafasi ya tatu na kusukuma Canada nafasi moja chini hadi nambari nne baada ya Wafaransa kupepeta Marekani 53-14 Julai 10. Marekani imesalia katika nafasi ya tano kwenye viwango hivi vinavyoongozwa na New Zealand. Uingereza ni nambari mbili. Zambia iliduwaza Zimbabwe 19-18 jijini Harare na kuingia katika viwango hivi vya mataifa 54 kwa mara ya kwanza kabisa. Wazambia wanashikilia nafasi ya 35. Zimbabwe imeteremka chini nafasi nne hadi nambari 41.

Katika viwango bora vya wanaume, ambavyo pia vinaongozwa na New Zealand, Kenya imekwamilia nafasi ya 32 duniani. Hata hivyo, imeongeza alama zake kutoka 50.05 hadi 52.25 baada ya kupepeta Uganda 16-5 katika mechi ya marudiano jijini Kampala.

Simbas ilikuwa imelimwa na Waganda 16-13 katika mechi ya mkondo wa kwanza. Ushindi wa Simbas umefanya Uganda kuteremka kutoka nafasi ya 35 hadi 39.

Hapo Julai 13, Kenya ilihifadhi mataji ya Elgon Cup baada ya Simbas na Lionesses kuzima Uganda kwa alama 16-5 na 33-5 mtawalia jijini Kampala.

Lionesses ya kocha Felix Oloo ilikuwa ya kwanza kutawazwa malkia ilipokamilisha kampeni safi iliyoanza na ushindi wa 42-13 mjini Kisumu mnamo Juni 22 na kukamilika kwa jumla ya alama 77-18 Julai 13.

Katika mechi ya marudiano Jumamosi, Grace Adhiambo alichangia penalti mbili na mkwaju, nahodha Philadelphia Olando akapachika miguso miwili nao Stella Wafula, Leah Wambui na Janet Okello wakafunga mguso mmoja kila mmoja. Kenya itakutana na Afrika Kusini, Madagascar na Uganda mwezi ujao katika mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Dunia mwaka 2021.

Simbas, ambayo ilikuwa chini ya kocha Albertus Van Buuren baada ya Paul Odera kusafiri nchini Brazil kwa Raga ya Dunia na timu ya Under-20 (Chipu), ilikuwa na kazi ngumu uwanjani Kyadondo.

Iliingia mechi hii ikiuguza kichapo cha alama 16-13 mjini Kisumu hapo Juni 22. Simbas ilianza vibaya mechi ya marudiano pale iliruhusu Uganda kuongoza 5-0 kupitia mguso bila mkwaju kutoka kwa Ronald Kanyanya. Nyota wa Kabras Sugar RFC Philip Wokorach alipoteza mkwaju.

Hata hivyo, Billy Omondi alisawazishia Kenya 5-5 kupitia pia mguso ambao Jacob Ojee hakufanikiwa kutinga mkwaju wake. Madhambi kutoka kwa Waganda yalimpa Ojee nafasi ya kuandikisha jina lake kwenye orodha ya wafungaji alipopachika penalti kwa ustadi na kuweka Kenya mbele 8-5.

Kenya haikulegeza kamba katika kipindi cha pili pale ilifungua mwanya hadi 11-5 kupitia penalti nyingine kutoka kwa Ojee ambaye alikamilisha ufufuo wa Simbas kupitia mguso baada ya kutimka mita 70 kutoka nusu ya Kenya alipopokea pasi murwa kutoka kwa Michael Wanjala.

Ingawa Ojee hakufaulu kuongeza mkwaju wa mguso huu, Kenya ilikuwa imepata alama za kutosha kutawazwa wafalme kwa mwaka wa nne mfululizo baada ya kunyakua mataji ya mwaka 2016, 2017 na 2018 bila kupoteza mechi.

Uganda, ambayo mara ya mwisho ilishinda Elgon Cup ni mwaka 2015, iliingia mechi ya marudiano ikiamini itarejesha taji. Hata habari kutoka Uganda zilisema kuwa Cranes ilikuwa imejiandaa kusherehekea taji kwa kuwapa mashabiki kreti 50 za bia ya aina ya Nile Special bila malipo.