• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 6:55 AM
Lionesses yaalikwa kushiriki Raga za Dunia nchini Canada

Lionesses yaalikwa kushiriki Raga za Dunia nchini Canada

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya raga ya wanawake ya Kenya almaarufu Lionesses imepata mwaliko kushiriki duru ya saba ya Raga za Dunia mjini Langford nchini Canada itakayofanyika Mei 2-3, 2020.

Lionesses ya kocha Felix Oloo imewahi kushiriki Raga za Dunia mara moja ilipoalikwa kushiriki duru ya Clermont-Ferrand nchini Ufaransa mwaka 2016 ikipoteza dhidi ya Uhispania 37-5, Uingereza 22-0 na Marekani 31-0 katika mechi za makundi na Urusi 27-12 katika mashindano ya Bakuli kabla ya kunyamazisha Japan 12-5 katika mechi ya kuamua nambari 11 na 12 (mwisho).

Mabingwa hao wa Kombe la Afrika mwaka 2018 walirejelea mazoezi Januari 6 baada ya likizo ya Krismasi.

Kabla ya kuelekea Canada, Lionesses itapata fursa ya kujaribu tena kufuzu kushiriki duru zote za Raga za Dunia itakapozuru Hong Kong mwezi Aprili. Ilijaribu kuingia Raga za Dunia mwaka 2016, 2017, 2018 na 2019, lakini bila mafanikio.

Lionesses, ambayo ilifuzu kushiriki Olimpiki 2020 baada ya kumaliza Kombe la Afrika 2019 katika nafasi ya pili nyuma ya Afrika Kusini, itatumia mashindano ya Hong Kong na Langford kujiandaa kwa michezo ya Olimpiki itakayofanyika Julai 27 hadi Agosti 1 mjini Tokyo nchini Japan.

  • Tags

You can share this post!

Mahakama yamuagiza Prof Kiama ajitenge na shughuli za...

China yatenga watu 30 milioni miji 10 kutokana na virusi

adminleo