Michezo

LIVERPOOL AU MAN-U? Vita vikali vya kuwania saini ya Bruno Fernandes

July 31st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

LISBON, Ureno

LIVERPOOL pamoja na mahasimu wao wakuu, Manchester United zimekutana katika vita vikali vya kuwania saini ya Bruno Fernandes wa Ureno. Lakini huenda United wakafaulu katika vita hivyo.

Nahodha huyo wa klabu ya Sporting Club Porto ya ligi kuu ya Ureno (Primeira Liga) tayari ametangaza thamani yake kuwa Sh9.3 bilioni.

Kocha Jurgen Klopp wa Liverpool kwa upande wake amekuwa akikanusha madai ya kumsajili kiungo huyo mahiri lakini imethibitishwa kwamba alionekana akizungumza naye wakati wa mechi ya kirafiki baina ya klabu yake na Sporting CP ziara nchini Amerika.

Kwa upande wa Manchester United, imesemekana kuwa tayari klabu hiyo ya Old Trafford imewasilisha ofa ya Sh8.2 bilioni kumtwaa staa huyo mwenye umri wa miaka 21, lakini imekataliwa.

Habari katika mitandao ya kijamii zimedai kwamba kumekuwa na ndege maalum kutoka Lisbon zikitua Manchester, hili likiwa thibitisho tosha kwamba huenda familia ya nyota huyo imeanza kuwasili nchini Uingereza.

United ilianza kumuandama staa huyo zaidi ya miaka miwili iliyopita na sasa imeona ndiye pekee anayeweza kujaza pengo la Paul Pogba anayejiandaa kuondoka.

Fernandes ni raia wa Ureno aliyezaliwa eneo la Maia mnamo Septemba 1994 na kucheza soka akiwa mdogo katika klabu ya Infesta kuanzia mwaka 2002.

Kufikia sasa, ameichezea Sporting CP mechi 66 na kuifungia mabao 31. Msimu uliopita aliichezea klabu hiyo mechi 33 na kufunga mabao 20, mbali na pasi alizotoa ambazo zilichangia kuingia kwa mabao 13.

Katika mechi hizo alicheza jumla ya dakika 2,943 ambapo kati ya penalti 11 alizopiga, alifungia 10 na kupoteza moja; kumaanisha penalti alizofunga ni sawa na asilimia 91.

Katika michuano ya Europa League msimu uliopita wa 2018/19 alicheza mechi nane, akafunga mabao matatu na kutoa pasi moja iliyozaa bao huku akicheza jumla ya dakika 703.

Bao moja

Kwa upande wa timu ya taifa ya Ureno, Fernandes ameichezea mechi 13 na kuifungia bao moja tu, huku katika michuano ya Klabu Bingwa barani Ulaya akicheza mechi tatu na kutumia dakika 171.

Wakati huo huo, mshambuliaji Raheen Sterling amesema kuwa mabingwa wa Ligi ya Klabu Bingwa barani Ulaya ni kitu muhimu kwa kila mwanasoka aliye na maono makubwa.

Nyota huyo aliyesaidia Mancester City kuhifadhi ubingwa wa ligi kuu ya Uingereza (EPL) kutokana na pointi 98, moja tu mbele ya Liverpool alisema alifurahia kuona klabu yake ya zamani, Liverpool ikitwaa ushindi wa taji la Ulaya.

Staa huyo mwenye umri wa miaka 24 aliondoka Merseyside mnamo 2015 katika mazingara ya kutatanisha alisema alifurahia kuona baadhi ya wachezaji aliocheza nao wakinyanyua taji hilo la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA)