• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 7:50 AM
Liverpool, Chelsea wafufuka muda ukiyoyoma huku Spurs wakizama

Liverpool, Chelsea wafufuka muda ukiyoyoma huku Spurs wakizama

NA MASHIRIKA

KOCHA wa Chelsea Mauricio Pochettino anasema, lengo lake sasa ni kufukuzia kushiriki katika mechi za Europa League msimu ujao, baada ya ushindi wa 5-0 dhidi ya West Ham Jumamosi katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Chelsea walipanda hadi nafasi ya saba kwenye msimo wa ligi na alama 54 baada ya mechi 35. Wana kibarua kingine dhidi ya Nottingham Forest wikendi ugenini.

The Blues imeshinda mechi tisa kati ya 11 zilizopita za EPL wakiwa nyumbani ambapo, wamepata ushindi mara tisa (sawa na Arsenal) na alama za nyumbani (28, sawa na Man City) kwenye kinyang’anyiro cha kuwania ubingwa wa EPL.

“Nina furaha sana kwa wachezaji na wafanyakazi wa timu hii baada ya ushindi dhidi ya Tottenham na kurudi tena baada ya siku chache na kupata ushindi mwingine. Nilifurahi sana jinsi tulivyoshindana Alhamisi na tuna wachezaji wenye vipaji vya kutengeneza nafasi na kufunga mabao,” alisema Pochettino.

Naye kocha wa West Ham David Moyes amewaomba msamaha mashabiki baada ya kichapo hicho.

West Ham wameruhusu mabao matano katika mechi zao mbili zilizopita za ugenini, wakiwa wamepoteza 5-2 dhidi ya Crystal Palace mnamo Aprili 21, na sasa wanakaribia kukosa msimu wa nne mfululizo katika mashindano ya Uropa.

Wameshinda mechi moja tu kati ya nane zilizopita za EPL, wakipoteza mara nne katika msururu huo – ingawa walitoka sare na Liverpool mara ya mwisho.

“Mashabiki wamekuwa wazuri lakini ninajisikia vibaya. Mashabiki wamejitokeza kwa wingi msimu huu na samahani sana kwa jinsi tulivyocheza. Tumekosa mabeki wazuri pia upande wa mashambulizi,” alielezea Moyes.

Kwa upande mwingine, Liverpool iliinyeshea Tottenham Hotspur 4-2 na kuendelea kuganda nafasi ya tatu kwenye jedwali na alama 78 alama tano nyuma ya vinara Arsenal huku Manchester City wakiwa nafasi ya pili na alama 82 wakiwa na mechi moja mkononi.

Wana uhakika wa kumaliza katika nafasi ya tatu, ingawa kihesabu bado wanaweza kushinda taji la EPL, ingawa City na Arsenal inafanya uwezekano huo kuwa ndoto.

Mbio za kujiunga na EPL

Mbio za kupanda daraja Ligi ya soka ya Uingereza (EFL) msimu huu ilishika kasi, huku Leicester City na Ipswich Town zikiwa ni timu za pekee kufikia sasa ambazo zimejikatia tiketi ya kushiriki EPL msimu ujao.

Leicester ya kocha Enzo Maresca ilimaliza nafasi ya kwanza kwenye jedwali na alama 97. Baada ya kuyumbayumba msimu jana, sasa wamefanikiwa kushinda taji na kupanda daraja.

Ipswich kwa upande mwingine, inajiunga na EPL baada ya miaka 22 na ilimaliza ya pili kwenye msimamo wa ligi na alama 96. Imepandishwa daraja tena mwaka mmoja tu baada ya kutoka Ligi ya Daraja la Kwanza.

Nani angetabiri hivyo?

The Tractor Boys wamekuwa na msimu mzuri chini ya Kieran McKenna na wamepanda daraja baada ya kuifunga Huddersfield Town katika mechi ya mwisho ya ligi Jumamosi ambapo walishinda 2-0.

Vilabu vingine tajika Leeds United, Southampton, West Brom na Norwich City, vikimaliza nafasi ya tatu, nne, tano na sita mtawalia na alama 90, 87,75 na 73 kila mmoja.

Katika ligi ya EFL, timu zinazomaliza nafasi ya tatu, nne, tano na sita zote zinashiriki mechi za mchujo wa kuwania Ubingwa.

Mchujo huo utahusisha Leeds ambayo itamenyana na Norwich City, nao West Brom itakabana koo dhidi ya Southampton.

  • Tags

You can share this post!

Uingereza yatoa fedha kusaidia Wakenya wanaohangaishwa na...

Wakazi wa Kisumu watahadharishwa ‘Nairobi fly’...

T L