Michezo

Liverpool kumsajili Ozan Kabak kujaza pengo la Van Dijk

October 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

LIVERPOOL wamefichua azma ya kumsajili beki chipukizi Ozan Kabak, 20, kutoka kambini mwa Schalke 04 ya Ujerumani mwanzoni mwa Januari 2021.

Kwa mujibu wa magazeti mengi nchini Uingereza, Liverpool wako tayari kuweka mezani kima cha Sh2.8 bilioni kwa minajili ya difenda huyo ambaye atajaza nafasi ya Virgil van Dijk atakayesalia mkekani kwa msimu mzima wa 2020-21 kwa sababu ya jeraha la goti.

Kocha Jurgen Klopp wa Liverpool amekuwa akitamani sana kujivunia huduma za Kabak na alijaribu kujinasia maarifa ya sogora huyo raia wa Uturuki mwishoni mwa msimu wa 2018-19.

Isingekuwa mkurupuko wa virusi vya corona, Liverpool walikuwa tayari kujitwalia huduma za Kabak katika muhula uliopita wa uhamisho wa wachezaji hata ingawa Schalke walisisitiza kwamba bei yake ni Sh5.6 bilioni.

Japo Schalke kwa sasa wametaka mnunuzi wa Kabak kuweka mezani Sh4.2 bilioni, Liverpool wamesema watakuwa radhi kuweka mezani Sh2.8 bilioni – awamu ya kwanza ya malipo ambayo yatafanikisha uhamisho wake mnamo Januari 2021 kabla ya salio kukamilishwa wakati wowote kuanzia Mei 2021.

Van Dijk hatarajiwi tena kurejea uwanjani msimu huu baada ya kupata jeraha baya alipokabiliwa visivyo na kipa wa Everton, Jordan Pickford katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyowakutanisha uwanjani Goodison Park mnamo Oktoba 17, 2020.

Kabak amekuwa mchezaji wa Schalke kwa zaidi ya mwaka mmoja uliopita baada ya kuagana na Stuttgart kwa kima cha Sh1.8 bilioni mwishoni mwa msimu wa 2018-19.

Akiwa mzawa wa Ankara, Kabak alianza kupiga soka ya kulipwa kambini mwa Galatasaray nchini Uturuki kabla ya kujiunga Schalke ya Ujerumani. Anajivunia pia kuchezea timu ya taifa ya Uturuki mara nne tangu awajibishwe kwa mara ya kwanza akiwa na umri wa miaka 14 pekee.

Van Dijk anatazamiwa kufanyiwa upasuaji wa goti mnamo Oktoba 27, 2020 na hofu kubwa zaidi kambini mwa timu ya taifa ya Uholanzi ni uwezekano wa kukosa huduma zake kwenye kipute cha Euro mwaka ujao wa 2021.