Michezo

Liverpool tuna kibarua kizito – Virgil van Dijk

October 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

BEKI Virgil van Dijk wa Liverpool amesema kwamba mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) watakabiliwa na upinzani mkali zaidi katika mechi zijazo kwa sababu kila kikosi kitatawaliwa na azma ya kuwaangusha.

Nyota huyo raia wa Uholanzi alikuwa sehemu muhimu katika kuchangia ufanisi wa Liverpool waliotwaa ubingwa wa EPL mwishoni mwa msimu wa 2019-20 baada ya kusubiri kwa miaka 30.

Kwa mujibu wa Van Dijk, ukosefu wa mashabiki uwanjani pamoja na matukio ya mara kwa mara ya ubaguzi wa rangi ambayo wachezaji wamekuwa wakikabiliwa nayo ni kati ya sababu ambazo pia zilichangia mwanzo mbaya wa Liverpool kwenye kampeni za EPL msimu huu.

“Sasa nimeanza Kuamini kwamba si kazi rahisi kudumisha nafasi ya kwanza kileleni mwa jedwali la EPL. Kila kikosi hujiandaa vilivyo kuzamisha dau la Liverpool uwanjani. Hivyo ndivyo mambo huwa maishani, hasa siku hizi katika mchezo huu wa soka,” akatanguliza sogora huyo wa zamani wa Southampton.

“Hata hivyo, nitajituma vilivyo na kujitolea hadi nitakapostaafu ili nisisumbuliwe tena na mawazo kama haya ya kukashifiwa kila mara kikosi kinapocheza vibaya au kupoteza mchuano wowote.”

“Sitaki kulaumiwa baadaye. Nitajitahidi kwa sababu nahisi hali itakuwa ngumu zaidi kwa Liverpool ambao ni mabingwa watetezi wa taji la EPL. Ni vyema kufurahia hilo, lakini lazima tujikaze zaidi katika mechi zijazo.”

“Tumezoea kucheza mbele ya idadi kubwa ya mashabiki, lakini kwa sasa mambo yamebadilika pakubwa ugani na hili ni jambo ambalo limewafanya baadhi ya wanasoka kulegea na kutepetea uwanjani,” akaongeza.

Tangu ashawishike kubanduka Southampton kwa Sh10.5 bilioni mnamo 2017, Van Dijk amesaidia Liverpool kutinga fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) katika msimu wa 2017-18 na pia katika EPL msimu wa 2018-19, kabla ya kutwaa mataji ya mashindano hayo misimu iliyofuata ya 2018-19 na 2019-20 mtawalia.

“Mashabiki ni kiungo muhimu sana uwanjani siku za mechi. Wao ndio huwapa wachezaji shime na moyo wa kujituma hata mnapofungwa na kujipata chini. Kelele zao ni za maana hata katika kushawishi marefa kufanya maamuzi fulani ya haki kwa jinsi inavyostahili.”

“Wanamtia mchezaji motisha zaidi kila wanapomshangilia kwa kufunga bao. Hilo ni jambo ambalo humpa mwanasoka yeyote nguvu na pumzi zaidi. Imekuwa vigumu kuchezea Anfield bila mashabiki. Tunatarajia mambo kubadilika ili hali ya kawaida irudi haraka iwezekanavyo,” akasema Van Dijk.