• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 10:55 AM
Liverpool wapaa Everton ikiingia mduara hatari

Liverpool wapaa Everton ikiingia mduara hatari

Na MASHIRIKA

HATA ingawa macho yalielekezwa kwa Liverpool iliyoendelea kupaa katika Ligi Kuu ya Uingereza, pana shujaa aliyestahili kusifiwa hata zaidi baada ya kuendelea kufanyia klabu yake vitu vya ajabu.

Kijana mwenye asili ya Kenya, Divock Origi alifunga mabao mawili na kusaidia Liverpool kubwaga Everton kwa mabao 5-2 yaliyomweka kocha Marco Silva katika hatari zaidi ya kufurushwa na klabu.

Gozi hilo la Merseyside la 234 lilishuhudia mabao sita katika kipindi cha kwanza. Wenyeji Liverpool waliona lango katika kipindi hicho kupitia kwa Divock Origi (mawili), Xherdan Shaqiri na Sadio Mane nao Michael Keane na Richarlison wakapachika mabao ya Everton. Liverpool ilihitimisha maangamizi hayo sekunde chache kabla ya mechi kutamatika kupitia kwa Georginio Wijnaldum.

Huku Liverpool ikiendelea kudhibiti nafasi yake ya kwanza na pia kudumisha rekodi ya kutoshindwa katika ardhi yake hadi mechi 20, Everton iliingia katika mduara hatari wa kutemwa na kumuacha Silva akikodolea macho kupigwa kalamu.

Bao la kwanza katika dakika 45 za kwanza za kusisimua lilifungwa na Liverpool baada ya Origi kuchenga kipa Jordan Pickford na kujaza katika nyavu tupu.

Mbelgiji huyo alikamilisha pasi murwa kutoka kwa Mane, ambaye pia alichangia bao la pili alipomegea Shaqiri pasi safi baada ya kupokea mpira kutoka kwa Trent Alexander-Arnold.

Hata hivyo, Liverpool, ambayo ilikuwa na kiu ya kuimarisha zaidi uongozi wake, ilisinzia kidogo na kupatia Everton nafasi ya kurejesha goli moja kupitia kwa Keane aliyemwaga kipa Adrian baada ya kupokea mpira mzuri ndani ya kisanduku.

Bao hilo lilifufua msukumo wa Everton timu hiyo, ambayo ilipoteza nafasi ya kusawazisha wakati Dominic Calvert-Lewin alipiga shuti nje alipopokea pasi kutoka kwa Alex Iwobi.

Kisha, Alexander-Arnold na Richarlison walionyeshwa kadi za njano, huku michecheto ikitishia kuvuruga mechi, ingawa haikuchukua muda kabla ya Liverpool kufungua pengo la magoli mawili tena.

Pasi ndefu kutoka kwa Dejan Lovren ilimpata Origi, ambaye alituliza vyema mpira kabla ya kusukuma kombora ndani ya kisanduku, ambalo Pickford hakuwa na lake.

Akamilisha shambulio la haraka

Zikisalia dakika nane kipindi cha kwanza kitamatike, Liverpool ilipata bao la nne kupitia kwa Mane, ambaye alikamilisha shambulio la haraka kutoka kwa Alexander-Arnold baada ya kuzima la Everton.

Wakiwa chini mabao 3-1, Silva alifanyia kikosi chake mabadiliko na pia mbinu, huku Bernard akijaza nafasi ya Djibril Sidibe timu ya Everton ikiamua kutumia mabeki wanne.

Mabadiliko haya yalizalisha matunda wakati Bernard alipiga krosi ambayo Richarlison alikamilisha kwa ustadi kupitia kichwa chake. Mengi yalitarajiwa kutoka kwa Everton katika kipindi cha pili, lakini ilifungiwa sana katika nusu yake.

Huku mashabiki wa Liverpool wakisherehekea ushindi huo wa mechi 14 kutoka 15 za ligi msimu huu, mashibiki wengi wa Everton walikuwa tayari wametoka uwanjani kipenga cha mwisho kilipolia baada ya kushuhudia timu yao ikiingia katika mduara hatari.

Leicester ilihakikisha mwanya kati yake na Liverpool unasalia alama nane baada ya kupepeta Watford 2-0 kupitia mabao ya Jamie Vardy (penalti) na James Maddison yaliyopatikana katika kipindi cha pili. Liverpool imezoa alama 43.

  • Tags

You can share this post!

Chapa Dimba yasaidia kijana kutimiza ndoto

Kenya yapoteza tena Dubai Sevens

adminleo