• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Liverpool wapiga Tottenham na kufungua mwanya wa alama tatu kileleni mwa jedwali la EPL

Liverpool wapiga Tottenham na kufungua mwanya wa alama tatu kileleni mwa jedwali la EPL

Na MASHIRIKA

BAO la dakika za mwisho kutoka kwa Roberto Firmino lilisaidia Liverpool kuzamisha chombo cha Tottenham Hotspur 2-1 katika mchuano wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumatano usiku.

Mechi hiyo ilionekana kukamilika kwa sare ya 1-1 hadi dakika ya 90 ambapo Firmino alikamilisha kwa kichwa krosi safi aliyopokezwa na beki Andrew Robertson.

Liverpool walifungiwa bao la kwanza na Mohamed Salah aliyeshuhudia kombora lake likimbabatiza beki Eric Dier kabla ya mpira kujaa wavuni mwa kipa Hugo Lloris katika dakika ya 26.

Bao hilo liliwazindua Tottenham waliosawazishiwa na Son Heung-min katika dakika ya 33 kabla ya kupoteza nafasi nyingi za wazi kupitia Steven Bergwijn na Harry Kane.

Ushindi wa Liverpool uliwaweka masogora hao wa kocha Jurgen Klopp kileleni mwa jedwali la EPL kwa alama 28, tatu zaidi kuliko Tottenham ambao wanatiwa makali na kocha raia wa Ureno, Jose Mourinho.

Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Tottenham kupoteza tangu wapokezwe kichapo cha 1-0 katika mechi ya kwanza ya msimu huu dhidi ya Everton.

Kabla ya kipenga cha kuashiria mwanzo wa mchuano huo kupulizwa, vikosi vyote viwili vilimkumbuka kocha wa zamani wa Liverpool, Gerard Houllier, aliyeaga dunia wiki hii akiwa na umri wa miaka 73.

Liverpool waliingia uwanjani kwa minajili ya mechi hiyo wakiwa na ulazima wa kujinyanyua baada ya kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya Fulham katika mechi ya awali.

Mabingwa hao watetezi wa EPL kwa sasa wanajivunia rekodi ya kutoshindwa katika jumla ya mechi 66 mfululizo kwenye EPL.

Aliposhuhudia Manchester United wakipigwa 3-1 na Tottehamn mnamo Disemba 2018 uwanjani Anfield, Mourinho alitimuliwa na waajiri wake saa 24 baadaye.

Tottenham sasa wameshinda mechi moja pekee kutokana na mechi 27 zilizopita za EPL dhidi ya Liverpool ambapo wamepigwa mara 18 na kuambulia sare mara nane. Mechi ya mwisho kwa Tottenham kushinda dhidi ya Liverpool ilikuwa Mei 2011.

Liverpool kwa sasa wanajiandaa kuwaendea Crystal Palace uwanjani Selhurst Park katika mechi ya EPL mnamo Disemba 19 huku Tottenham wakiwaalika Leicester City siku moja baadaye.

You can share this post!

Real Sociedad yaondoka kileleni mwa jedwali la La Liga...

Fida yawashikisha adabu Aisha Jumwa na Edwin Sifuna