Michezo

Liverpool yazima ndoto ya Bayern Munich

March 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

MATUMAINI ya klabu kutoka Uingereza kushinda Klabu Bingwa Ulaya kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2012 yaliongezeka pale Liverpool ilipokamilisha orodha ya wawakilishi wote wanne kutoka nchi hiyo waliotinga robo-fainali ilipozima Bayern Munich 3-1 Jumatano usiku nchini Ujerumani.

Tottenham Hotspur, Manchester United na Manchester City ziliingia mduara wa nane-bora baada ya kubandua nje Wajerumani Borussia Dortmund (Machi 5), Wafaransa Paris Saint-Germain (Machi 6) na Wajerumani Schalke 04 (Machi 12), mtawalia.

Inamaanisha kwamba timu zote za Uingereza bado zimo mbioni kufuata nyayo za Chelsea iliyoibuka mfalme mwaka 2012.

Tangu mwaka 2013, timu kutoka Uhispania zimetawala mashindano haya ya kifahari, ambayo mshindi huingia Kombe la Dunia la Klabu. Klabu kutoka Uhispania zimeshinda mataji matano kati ya sita yaliyopita.

Wajerumani Bayern walinyakua ubingwa wa mwaka 2013, Real Madrid mwaka uliofuata na Barcelona mwaka 2015 kabla ya Madrid kushinda makala matatu yaliyopita. Hata hivyo, Madrid, ambayo inashikilia rekodi ya mataji mengi ya Klabu Bingwa (13), haimo mbioni baada ya kukung’utwa na Ajax Amsterdam kutoka Uholanzi kwa jumla ya mabao 5-3 katika raundi ya 16-bora.

Liverpool na Barcelona zilikuwa timu za mwisho kuingia robo-fainali baada ya kubwaga Bayern na Lyon mtawalia, Jumatano. Klabu zingine katika robo-fainali ni Juventus anayochezea mvamizi matata Cristiano Ronaldo na Porto.

Mabingwa wa mwaka 1985 na 1996 Juventus walibandua nje Atletico Madrid kwa jumla ya mabao 3-0, mabao yaliyofungwa na Ronaldo katika mechi ya marudiano.

Uwanja wa nyumbani wa Atletico, Wanda Metropolitano, utatumika katika fainali Juni 1.

Porto ilizamisha Waitaliano AS Roma kwa jumla ya mabao 4-3.

Barcelona ilizima Wafaransa Lyon kwa jumla ya mabao 5-1 yaliyopatikana katika mechi ya mkondo wa pili.

Lionel Messi alifunga mabao mawili, moja kupitia penalti, na kumega pasi mbili zilizofungwa Gerard Pique na Ousmane Dembele naye Phillippe Coutinho akachangia bao moja.

Lucas Tousart alifungia Lyon bao la kufutia machozi.

Mabingwa mara tano Liverpool, ambao walishinda kombe hili mara ya mwisho mwaka 2005, walionyesha wana kiu ya kushindania taji walipozamisha washindi mara tano Bayern kupitia mabao mawili ya Sadio Mane na moja kutoka kwa Virgil van Dijk uwanjani Allianz Arena.

“Ni hatua kubwa kurejesha klabu hii katika ulingo wa Bara Ulaya na ninafurahia sana,” alisema kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp.

“Kama Barcelona ama Real Madrid watakuja hapa, wanajua ni mahali pagumu pa kupata ushindi.

“Ni hatua kubwa kwetu, wacha tuone tunaitumia kivipi, lakini tumeonyesha wazi kwamba tumerejea juu ya soka ya kimataifa.

“Tunafikiri hapa ndipo klabu inastahili kuwa, lakini wacha tuendelee, tuna mengi ya kujifunza, mengi ya kuimarisha, lakini tumerejea.”

Van Dijk atoa mchango mkubwa

Baada ya kukosa mechi ya mkondo wa kwanza uwanjani Anfield wiki tatu zilizopita akitumikia marufuku, pasi ndefu za Van Dijk zilichangia katika bao safi lililofungwa na Mane.

Beki huyu Mholanzi kisha aliweka Liverpool mbele 2-1 alipokamilisha kona ya James Milner baada ya Joel Matip kufungia Bayern kwa kujifunga.

Mane alihakikishia Liverpool tiketi ya robo-fainali alipofuma bao lake la pili kupitia kichwa zikisalia dakika sita mechi kutamatika.

Ni mara ya kwanza wawakilishi wote wa Uingereza wamefika robo-fainali tangu msimu 2008-2009.

Nayo Ujerumani haina timu katika robo-fainali kwa mara ya kwanza tangu msimu 2005-2006.

Pia, ni mara ya kwanza Bayern imeshindwa kuingia robo-fainali tangu mwaka 2011.