Michezo

LONDON MARATHON: Sababu za washindi kutuzwa takriban nusu ya hela zilizotolewa 2019

October 6th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

MSHIKILIZI wa rekodi ya dunia katika mbio za marathon, Brigid Kosgei, alitetea ubingwa wake wa taji la London Marathon kwa kufikia utepeni akiwa wa kwanza baada ya muda wa saa 2:18:58.

Kosgei, 26, alitia mfukoni takriban Sh3.2 milioni kwa ushindi huo uliomshuhudia akiwabwaga Sara Hall wa Amerika na bingwa wa dunia, Ruth Chepng’etich.

Sh3.2 milioni ambazo Kosgei alipokezwa zilipungua kwa Sh2.3 milioni hasa ikizingatiwa kwamba alituzwa Sh5.5 milioni alipoibuka mshindi wa London Marathon katika makala ya 39 mnamo 2019.

Kwa mujibu wa kanuni mpya za London Marathon mwaka 2020, kiasi sawa cha fedha kilitolewa pia kwa washindi wa mbio hizo za kilomita 42 kwa upande wa wanaume.

Miezi michache kabla ya kuandaliwa kwa mbio hizo mnamo Oktoba 4, 2020, waandalizi walisema kwamba fedha ambazo zingetolewa kwa washindi wa London Marathon zingepunguzwa kwa takriban asilimia 50 kutoka tuzo iliyokuwa ikitolewa awali kwa sababu ya janga la corona lililotikisa pakubwa sekta za michezo mbalimbali kifedha.

Waandalizi walisisitiza kwamba Covid-19 ilitatiza pakubwa kalenda ya michezo kote duniani na kulemaza hazina ambazo vinginevyo wasimamizi wa mashindano mbalimbali wangalipata kama hakungalikuwepo changamoto zilizozuliwa na virusi vya corona.

Mbio za London Marathon ambazo zilikuwa ziandaliwe mnamo Aprili 2020 kabla ya kuahirishwa kwa sababu ya corona, zilishirikisha wanariadha wa haiba kubwa pekee duniani.

Kinyume na hali ilivyo katika miaka ya awali ambapo washiriki wangekimbia barabarani, wanariadha walitakiwa kupiga jumla ya mizunguko 20 kwenye eneo lililozingirwa uwanjani St James’ Park, Uingereza mwaka 2020.

London Marathon ndiyo ya pekee iliyoandaliwa mwaka huu baada ya marathon za Boston, New York, Chicago na Berlin kufutiliwa mbali.

Kusitishwa kwa Berlin Marathon iliyokuwa ifanyike Septemba 27, 2020 kulitokana na hatua ya serikali ya Ujerumani kupiga marufuku mikusanyiko yote ya umma hadi Oktoba 24. New York City Marathon ilikuwa imeratibiwa kutifuliwa Novemba 1, 2020.

Kufutiliwa mbali kwa Riadha za Great North Run na Berlin Marathon zilizotazamiwa kuandaliwa Septemba 2020, kuliibua pia utata na suitafahamu kuhusu uwezekano wa kuandaliwa kwa London Marathon.

Kiini cha kufutiliwa mbali kwa mbio Great North Run ni changamoto za kutekeleza baadhi ya kanuni mpya za afya zinazolenga kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19, hasa masharti ya kudumisha umbali wa hadi mita moja kati ya watu.

Kwa kawaida, mbio za London Marathon hushirikisha zaidi ya wanariadha 45,000. Mnamo 2019, jumla ya Sh9.2 bilioni zilichangishwa kutokana na London Marathon. Fedha hizo zilitumiwa katika shughuli za hisani kote duniani.