Lucy Wangui agunduliwa kuwa mtumizi sugu wa pufya
Na GEOFFREY ANENE
ZIMWI la wanariadha kutumia njia ya mkato kutafuta ufanisi mashindanoni linazidi kuandama Kenya baada ya Lucy Wangui Kabuu kuwa mkimbiaji wa hivi punde kufeli vipimo vya dawa zilizoharamishwa.
Bingwa huyu Jumuiya ya Madola wa mbio za mita 10,000 mwaka 2006 amepatikana na kosa la matumizi ya pufya katika mbio za Milano Marathon alizoshinda nchini Italia mwezi Aprili mwaka 2018. Alipimwa wakati wa mbio hizo na matokeo tayari yamefikishwa kwake.
Mzawa huyu wa mwaka 1984 hakuwa amepata ushindi mkubwa kama huo wa Milano Marathon katika mbio za kilomita 42 katika historia yake. Alinyakua taji la Milano miezi miwili baada ya kupona jeraha. Aliwahi kushinda mbio za kilomita 21 za Delhi Half Marathon nchini India mwaka 2011, Ras Al Khaimah Half Marathon nchini Milki za Kiarabu (2013) na Great North Run nchini Uingereza (2011).
Kenya, ambayo ilishuhudia karibu visa 50 kati ya mwaka 2012 na 2016, iliingia kwenye orodha ya mataifa yanayotenda uovu huu sana ya Shirika la Kukabiliana na matumizi ya dawa za kusisimua misuli (WADA) mnamo Mei 12 mwaka 2016. Bado inakabiliwa na tishio la kupigwa marufuku kushiriki mashindano kimataifa kama Urusi.
Kisa cha Kabuu kinawasili wiki chache baada ya wakimbiaji wengine watajika kutoka Kenya, Asbel Kiprop (mita 1,500) na Boniface Mweresa (mita 400) kupatikana watumiaji wa dawa hizo haramu. Kutokana na uhalifu huu, Kiprop, Mweresa na Kabuu wanakabiliwa na marufuku ya miaka minne kutoka kwa Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF).