Michezo

Luis Enrique afananisha soka bila mashabiki uwanjani na densi ya mtu na dada yake

May 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Luis Enrique wa timu ya taifa ya Uhispania amesema kwamba kucheza mpira ndani ya viwanja vitupu bila mashabiki hakuna ladha kabisa na “kunasikitisha zaidi kuliko kusakata densi na dadako.”

Kampeni za Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) zilianza upya wikendi ya Mei 16, 2020 na kufanya kipute hicho kuwa cha kwanza kurejelewa miongoni mwa tano kuu katika soka ya bara Ulaya.

Zaidi ya mashabiki kutokubaliwa uwanjani, wachezaji wa ziada, makocha na maafisa wa vikosi husika wamesisitiziwa haja ya kudumisha umbali wa mita moja na nusu kati yao huku wanaofunga mabao wakitakiwa kutosherehekea kwa kusalimiana wala kupigana pambaja.

“Soka tena haina ladha. Inaudhi sana. Ni sawa na kucheza ngoma na dadako mkishikana,” akatanguliza kocha huyo wa zamani wa Barcelona.

“Nilitazama mechi za Bundesliga wikendi iliyopita na picha iliyochereka uwanjani ilikuwa ya kusikitisha sana. Mtu angalisikia wachezaji wakitusiana vibaya. Ni miongoni mwa matukio yanayomwondolea mtu hamu ya kufuatilia mchezo ambao unapendwa sana duniani kote,” akasema Enrique, 50.

Hata hivyo, Enrique alisema kwamba anaelewa kiini cha kandanda ya soka kuchezewa chini ya kanuni zilizowekwa katika juhudi za kudhibiti maambukizi zaidi ya virusi vya homa kali ya corona.

“Soka ni biashara kubwa inayovunia mataifa mengi mabilioni ya pesa na kuchangia maendeleo. Japo haipendezi sana kuitazama kwa sasa, inasaidia kuwaondolea watu msongo wa mawazo kutokana na gonjwa hili la corona.”