• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
Luis Suarez sasa ni mali ya Atletico Madrid

Luis Suarez sasa ni mali ya Atletico Madrid

Na MASHIRIKA

MADRID, Uhispania:

Ni rasmi sasa kuwa Luis Suarez ni mali ya Atletico Madrid baada ya kuagana na Barcelona hapo Alhamisi.

Mshambuliaji huyo wa Uruguay anaaminika aliitishia kuanika siri ya Barca kuhusu orodha ya klabu ambazo miamba hao wa Uhispania walikuwa wamemkataza asihamie.

Suarez sasa amepata hifadhi mpya Atletico baada ya kununuliwa kwa bei ya kupunguzwa ya Sh760 milioni.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33 alikuwa amehusishwa sana na uhamisho hadi Juventus nchini Italia.

Suarez alitokwa na machozi katika kipindi chake cha mwisho cha mazoezi uwanjani Camp Nou majuzi alipoambiwa na kocha mpya Ronald Koeman kuwa Barca haihitaji huduma zake tena.

Gazeti la Mundo Deportivo nchini Uhispania linadai kuwa makubaliano ya kuhamia Atletico yaliharakishwa baada ya Suarez kutisha kuwa atasambaza barua-pepe kutoka kwa Barcelona iliyomtajia klabu ambazo haitaki ahamie bila kulipia ada ya uhamisho. Atletico inasemekana haikuwa katika orodha hiyo.

Tangu ajiunge na Barca akitokea Liverpool mwaka 2014, Suarez ameshinda mataji mengi ikiwemo Klabu Bingwa Ulaya mwaka 2015 na mataji manne ya Ligi Kuu ya La Liga.

Anaondoka Camp Nou akiwa mfungaji wa tatu bora baada ya kuchana nyavu mara 198. Supastaa Lionel Messi na Cesar Rodriguez wanashikilia nafasi mbili za kwanza baada ya kufungia Barca mabao 634 na 232, mtawalia.

Kujiunga kwake na mahasimu hao wa Barcelona kwenye La Liga kunafuatia kusambaratika kwa mpango wa kuhamia Juventus.

Kocha wa Juventus, Andrea Pirlo alifichua juma lililopita kuwa matumaini ya kupata huduma za Suarez ni finyu kwa sababu ya mpango wa mchezaji huyo kuwa raia wa Italia kucheleshwa.

Mnamo Septemba 22, waendesha mashtaka mjini Perugia nchini Italia walisema walituhumu Suarez kwa kufanya udanganyifu kupita mtihani wake wa umilisi wake wa lugha ya Kitaliano kwa kusaidiwa na waliosimamia mtihani wake.

TAFSIRI: GEOFFREY ANENE

  • Tags

You can share this post!

Kazuyoshi Miura avunja rekodi ya uzee ligini Japan

Ithibati tosha Diego Simeone anapenda wachezaji watundu