Lukaku ataka Fifa kuadhibu wanaoeneza ubaguzi wa rangi
Na AFP
SARDEGNA ARENA, ITALIA
MSHAMBULIZI mpya wa Inter Milan, Romelu Lukaku, amelitaka Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) kuchukua hatua kali dhidi ya mashabiki wanaoendeleza ubaguzi wa rangi kwa sababu tabia hiyo inarejesha nyuma mchezo wa kabumbu.
Fowadi huyo raia wa Ubelgiji alitusiwa, akakejeliwa na hata kuitwa nyani na mashabiki wa Cagliari FC siku ya Jumapili wakati wa mechi ya Serie A baina ya timu hizo mbili ugani Sardegna Arena.
Lukaku ambaye alihamia Inter Milan kutoka Manchester United ya Uingereza, alikumbana na matusi hayo ya ubaguzi wa rangi alipokuwa akijiandaa kuchanja penalti kwenye lango la Cagliari, mkwaju ambao aliishia kuufunga na kuchangia ushindi wa 2-1 kwa timu yake.
Kinaya ni kwamba ni uga uo huo ambapo wanasoka nyota Moise Kean, Blaise Matuidi na Sulley Muntari ambao wana asili ya kiafrika pia walimiminiwa matusi ya kukejeli rangi ya miili yao miaka ya nyuma.
Tayari kitengo cha nidhamu cha Serie A kimeanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo na kuahidi kwamba mashabiki waliohusika wataadhibiwa vikali ili kutoa mfano kwa wengine wanaoendeleza ubaguzi huo.
Hata hivyo, Lukaku mwenyewe alisikitikia tukio hilo na kusema ubaguzi wa rangi ni tatizo ambalo halifai kuvumiliwa enzi hizi ambazo mchezo wa kabumbu umepiga hatua kubwa duniani.
“Wachezaji wengi walikumbana na ubaguzi wa rangi mwezi uliopita kutoka kwa mashabiki. Nilijipata kwenye hali hiyo Jumapili, kwa kweli inasikitisha sana,” akaandika Lukaku kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii Instagram.
“Soka ni mchezo ambao unaburudisha kila mtu na tabia zozote za ubaguzi hazifai kuvumiliwa kamwe. Ubaguzi wa rangi ni aibu kwenye soka na nina matumaini kwamba FIFA na Mashirikisho mengine ya soka duniani yatafanya juu chini kuhakikisha unatokomezwa kabisa,” akasema Lukaku.
Tukio hilo la Jumapili linajiri baada ya waliokuwa wachezaji wenza wa Lukaku, Marcus Rashford na Paul Pogba pamoja na wanasoka wa Chelsea Tammy Abraham na Kurt Zouma kurushiwa matusi ya ubaguzi wa rangi kwenye mitandao ya kijamii na mashabiki wa timu pinzani kwenye mechi zilizopita za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).
Aidha Lukaku alisema mitandao ya kijamii ambayo inatumika kueneza ubaguzi wa rangi pia inafaa kudhibitiwa, akifunguka na kusema yeye binafsi ameathiriwa sana na matusi aliyorushiwa Jumapili.
“Mitandao ya kijamii kama Facebook, Instagram, na Twitter inafaa kushirikiana na klabu za soka kwa sababu kila siku hapakosi chapisho la ubaguzi wa rangi. Tumekuwa tukisisitiza kwamba hili halifai lakini hakuna kinachobadilika.”