Michezo

Mabadiliko machache 'Ghost' Mulee akitaja kikosi cha Harambee Stars atakachokitegemea dhidi ya Comoros

October 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA mpya wa Harambee Stars, Jacob ‘Ghost’ Mulee ametaja kikosi cha wanasoka atakaowategemea katika mechi mbili zijazo dhidi ya Comoros katika vita vya kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) 2021.

Stars wameratibiwa kuwa wenyeji wa Comoros mnamo Novemba 11 jijini Nairobi kabla ya kurudiana na Wanavisiwa hao mjini Moroni siku nne baadaye.

Kati ya wanasoka ambao Mulee amewapa fursa ya kudhihirisha ukubwa wa uwezo wao uwanjani ni kipa Brian Bwire wa Kariobangi Sharks na Robert Mboya wa Tusker FC. Wawili hao watakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Arnold Origi wa HIFK Fotboll (Finland), Ian Otieno wa Zesco United (Zambia) na Timothy Odhiambo wa Ulinzi Stars (Kenya).

Daniel Sakari wa Sharks amejumuishwa pamoja na Andrew Juma (Gor Mahia) na Michael Kibwage (Sofapaka) katika orodha ya mabeki watakaotegemewa na Stars.

David ‘Calabar’ Owino wa Zesco United pia amepokezwa fursa ya kudhihirisha ubabe wake kwa mara nyingine katika timu ya taifa.

Kati ya wanasoka wanaorejea katika kikosi cha Stars baada ya kuwa nje kwa kipindi kirefu ni Ismael Gonzalez anayechezea Las Palmas ya Uhispania na Boniface Muchiri wa Tusker ambao ni mabingwa mara 11 wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL).

Wengine ambao wamepata fursa ya kunogesha soka chini ya Mulee aliyejaza pengo la Francis Kimanzi mnamo Oktoba 21, 2020 ni Elly Asieche, limbukeni Mathew Olake na sajili mpya wa AFC Leopards, Peter Thiong’o.

Wachezaji wanaosakata soka katika klabu mbalimbali za ligi ya humu nchini wanatarajiwa kuripoti kambini mnamo Oktoba 28 huku wale wanaotandaza kabumbu ya kulipwa ughaibuni wakitazamiwa kuingia kambini kufikia Novemba 2, 2020. Ni wachezaji 20 pekee ambao watajumuishwa kwenye orodha ya mwisho ya masogora watakaotegemewa na Mulee dhidi ya Comoros.

Chini ya Kimanzi, Stars walianza kampeni zao za Kundi G kufuzu kwa fainali zijazo za AFCON dhidi ya Misri kwa sare ya 1-1 mnamo Novemba 14, 2019 ugenini kabla ya kusajili matokeo sawa na hayo dhidi ya Togo mnamo Novemba 18, 2019 jijini Nairobi.

KIKOSI CHA STARS:

MAKIPA: Arnold Origi (HIFK, Finland), Robert Mboya (Tusker, Kenya), Brian Bwire (Kariobangi Sharks, Kenya), Ian Otieno (Zesco United, Zambia), Timothy Odhiambo (Ulinzi Stars, Kenya).

MABEKI: Johnstone Omurwa (Wazito, Kenya), Brian Mandela (hana klabu), Joash Onyango (Simba, Tanzania), Daniel Sakari (Kariobangi Sharks, Kenya) Andrew Juma (Gor Mahia, Kenya), Mike Kibwage (Sofapaka, Kenya), Joseph Okumu (Elfsborg, Uswidi), Samuel Olwande (Kariobangi Sharks, Kenya), Baraka Badi (KCB, Kenya), David Owino (Zesco United, Zambia), Hillary Wandera (Tusker, Kenya), Eric Ouma (AIK, Uswidi), David Owino (Mathare United, Kenya).

VIUNGO: Kenneth Muguna (Gor Mahia, Kenya), Victor Wanyama (Impact Montreal, Canada), Ismael Gonzalez (UD Las Palmas, Uhispania), Eric Johanna Omondi (Jonkoping’s Sodra, Uswidi), Cliff Nyakeya (Masr FC, Misri), Antony Akumu (Kaizer Chiefs, Afrika Kusini), Musa Masika (Wazito, Kenya), Bonface Muchiri (Tusker, Kenya) Lawrence Juma (Sofapaka, Kenya), Johanna Omolo (Cercle Brugge, Ubelgiji), Ayub Timbe (hana klabu), Peter Thiong’o (AFC Leopards, Kenya), Hassan Abdallah (Bandari, Kenya), Elli Asieche (Sofapaka, Kenya), Mathew Olake (hana klabu), Moses Mudavadi (Kakamega Homeboyz, Kenya), Austin Odhiambo (AFC Leopards, Kenya).

WAVAMIZI: Michael Olunga (Kashiwa Reysol, Japan), Benson Omala (Gor Mahia, Kenya), Masud Juma (JS Kabylie, Algeria), John Avire (Tanta FC, Misri), Oscar Wamalwa (Ulinzi Stars, Kenya).

WACHEZAJI WA AKIBA: Dennis Sikhayi (Wazito, Kenya), James Kinyanjui (Mathare United, Kenya).