Michezo

Mabilioni ya SportPesa yanarejea?

July 1st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

KAMPUNI ya kamari ya SportPesa imeashiria inapanga kurejea katika soko la Kenya, saa chache tu baada ya Rais Uhuru Kenyatta kusaini mswada wa fedha Juni 30, 2020.

Baada ya serikali kulegeza msimamo wake hapo Juni 30 kuhusu ushuru wenye utata unaotozwa kampuni hizo na watu wanaobashiri mechi na ambao ulichangia kampuni nyingi kujiondoa soko la Kenya, SportPesa ilichapisha ujumbe kwenye mtandao wake wa Twitter wa kupatia wateja wake matumaini.

Ikijibu mteja AChevinar aliyeuliza kama itarejea Kenya, SportPesa ilisema, “Hatuna tarehe rasmi tutakayorejelea shughuli zetu, lakini tuna matumaini ya kufanya hivyo.”

Mswada huo, ambao umefanyiwa marekebisho, unaondoa ushuru utata uliochangia SportPesa na ile ya Betin na nyinginezo kujiondoa Kenya miezi tisa iliyopita.

Kabla ya kujiondoa kabisa katika soko la Kenya mnamo Septemba 2019, SportPesa ilikuwa ikidhamini Gor Mahia, AFC Leopards, Ligi ya Ndondi, Shirikisho la Raga Kenya, Kenya Harlequin, Ligi Kuu ya Soka ya Kenya na pia mashindano ya kimataifa kati ya klabu za soka za Kenya na Tanzania pamoja na kuleta klabu ya Uingereza Everton nchini Kenya na Tanzania na Hull City nchini Kenya, miongoni mwa shughuli zingine. Pia, ilikuwa imeajiri mamia ya Wakenya katika afisi zake jijini Nairobi.

SportPesa ilikuwa mstari wa mbele kupinga sheria kali za kutozwa ushuru wa asilimia 35 zilizopitishwa na serikali. Kampuni hiyo inasemekana ilipokea Sh20 bilioni kila mwezi kutokana na beti ambazo Wakenya walikuwa wakiwekeza wanapobashiri mechi za Kenya na mataifa mengine, wakitafuta kujishindia fedha.

Kampuni hiyo, ambayo ilianza shughuli zake Kenya mwaka 2014, ilikuwa ikitawala asilimia 64 ya soko la humu nchini. Ilisalia na katika mataifa ya Tanzania, Afrika Kusini, Italia, Ireland, Isle of Man na Uingereza baada ya kujiondoa Kenya.

Betin inaaminika ilitawala soko la Kenya kwa asilimia 20 ikifuatiwa na Betika, Betpawa Sportybet, mtawalia. Kampuni hizi zilikuwa katika orodha ya 27 za kamari zilizopokonywa leseni Julai 2019 na Bodi ya Kudhibiti na Kutoa Leseni nchini (BCLB) kwa masuala yanayohusiana na ushuru.

Betika haikuondoka Kenya. Kwa sasa, inaongoza soko hili ikijiuza kupitia kwa Ligi ya Supa. Betsafe ilijitosa nchini Kenya wiki chache zilizopita ilipotangaza kusaini kandarasi na klabu mbili kongwe za soka Gor Mahia na AFC Leopards kwa kuzidhamini Sh55 milioni na Sh40 milioni kila mwaka kwa kipindi cha miaka mitatu.