Michezo

Macho kwa Kiprotich kwenye urushaji mkuki Kip Keino Classic

October 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

MSHINDI wa nishani ye fedha katika fani ya urushaji mkuki barani Afrika, Alexander Kiprotich, sasa ana kibarua kizito cha kuweka hai matumaini ya kutambisha Kenya kwenye mashindano ya Kip Keino Classic mnamo Oktoba 3, 2020 baada ya kujiondoa kwa bingwa wa zamani wa dunia, Julius Yego.

“Kujiondoa kwa Yego kutokana na jeraha ni pigo kubwa. Hata hivyo, nitajituma kadri ya uwezo na kusajili matokeo bora japo natarajia ushindani mkali kutoka kwa Timothy Herman wa Ubelgiji,” akasema Kiprotich.

Kiprotich amekuwa akijifanyia mazoezi tangu kusitishwa kwa shughuli zote za michezo humu nchini mnamo Machi 2020 kwa sababu ya janga la corona.

“Corona iliathiri pakubwa ratiba yangu ya kujifua. Viwanja vingi vilifunguliwa chini ya kipindi cha mwezi mmoja uliopita. Hivyo, sijapata muda bora zaidi wa kujinoa ipasavyo,” akasema.

Kiprotich, ambaye ni mwanajeshi, analenga kutumia mashindano ya Kip Keino Classic kuwa jukwaa mwafaka zaidi la kujiandalia kwa michezo ya Olimpiki ya 2020 jijini Tokyo, Japan.

Kiprotich aliambulia nafasi ya pili nyuma ya Yego katika Miecho ya Afrika mnamo 2019 jijini Rabat, Morocco (77.50m) huku Yego akirusha mkuki hadi umbali wa mita 87.73.

Uwanjani Nyayo, Nairobi, Kiprotich ambaye kwa sasa ananolewa na kocha Joseph Mosonik, atawaongoza Wakenya wengine Duncan Kinyanjui na Methusellah Kiprop.

Fani hiyo ya urushaji mkuki imewavutia pia Timothy Herman, Dominik Sokola (Hungary), Lukas Moutarde (Ufaransa), Hubert Chmielak (Poland) na Johann Grobler wa Afrika Kusini.

“Johann Grobler wa Afrika Kusini ndiye tishio kubwa zaidi katika fani hiyo. Kiprotich bado hajarejelea ubora wake kabisa. Pengine yuko katika hatua ya asilimia 75 ya ubora sasa,” akasema Mosonik ambaye pia humnoa Yego.

Yego anatarajiw akurejea ugani kwa matao ya juu mwaka ujao katika Olimpiki za Tokyo na pia kunogesha Mashindano ya Dunia yatakayoandaliwa jijini Oregon, Amerika mnamo 2021.