Michezo

Macho ya Wakenya kwa Timothy Cheruiyot mbio za Diamond League mjini Lausanne

July 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

BINGWA wa Riadha za Diamond League, duru ya Uswidi na Amerika, Timothy Cheruiyot ni mmoja wa wakimbiaji wanaotarajiwa kupeperusha bendera ya Kenya vilivyo baada ya orodha kutoka ya washiriki wa duru ya mjini Lausanne nchini Uswizi leo Ijumaa Julai 5, 2019.

Cheruiyot atalenga kusalia juu ya jedwali la mbio za mita 1,500 anazoongoza kwa alama 23, pointi 12 mbele ya Michael Rodgers wa Amerika.

Mkimbiaji huyu mwenye umri wa miaka 23, ambaye alishinda Riadha Diamond League mwaka 2017 na 2018 atapata ushindani mkali kutoka kwa Wakenya wenzake Bethwell Brigen, Vincent Kibet, Boaz Kiprugut, Ronald Kwemoi, Timothy Sein na Justus Soget pamoja na wakimbiaji kutoka Norway, Uhispania, Uganda, Djibouti, Uingereza na Ethiopia.

Kwa jumla, Wakenya wanatarajiwa kuwa na kibarua kigumu mjini Lausanne.

Katika mbio za mita 5,000 ambazo zimevutia wakimbiaji 25, Kenya ina wakimbiaji Richard Yator, Paul Tanui, Davis Kiplangat, Cornelius Kangogo na Nicholas Kimeli.

Kuna majina makubwa hapa yatakayotoa Wakenya kijasho yakiwemo Joshua Cheptegei (Uganda) na Waethiopia Edris Muktar, Hagos Gebrhiwet, Selemon Barega na Yomif Kejelcha.

Bingwa wa Jumuiya ya Madola Wycliffe Kinyamal pamoja na Emmanuel Korir na Ferguson Rotich kutoka Kenya pia wanatarajiwa kutolewa kijasho katika mbio za mita 800. Watakutana na Brandon McBride (Canada), ambaye ametimka 1:43.90 msimu huu.

Rotich, Korir na Kinyamal wamekamilisha umbali huo kwa dakika 1:44.11, 1:44.50 na 1:44.65 msimu huu, mtawalia. Kitengo hiki kimevutia wakimbiaji 11 wakiwemo Wesley Vazquez (Puerto Rico), Amel Tuka (Bosnia & Herzegovina) na Clayton Murphy (Marekani) ambao pia wako katika orodha ya wakimbiaji wanaopigiwa upatu kutwaa ubingwa.

Nao Nelly Jepkosgei na Mary Kuria watashiriki mbio za mita 800, ambazo zimevutia wakimbiaji 11 kutoka mataifa ya Kenya, Uswizi, Slovakia, Uswidi, Uganda, Latvia, Lithuania na Ethiopia.

Muda bora wa Jepkosgei katika mbio hizi za mizunguko miwili ni dakika 1:58.96. Ametimka umbali huo kwa 1:59.00 msimu huu, kasi ambayo ndiyo bora kuliko wapinzani wake.

Kutokana na muda huo, Jepkosgei ataanza na asilimia kubwa ya kutwaa taji. Hata hivyo, ushindani mkali unatarajiwa kutoka kwa Gabriela Gajanova (Slovakia) na Halimah Nakaayi (Uganda) wanaojivunia muda wa dakika 2:00.58 kila mmoja msimu huu.