Magelo aitisha kikao kuokoa soka nchini
Na JOHN ASHIHUNDU
ALIYEKUWA mwenyekiti wa klabu ya AFC Leopards, Alex Ole Magelo ametoa wito kwa washikadau wa soka nchini wakutane haraka iwezekanavyo kupanga mikakati itakayookoa mchezo huo baada ya Jopo la Kutatua Mizozo Michezoni (SDT) kufutilia mbali uchaguzi wa Shirikisho la Soka Nchini (FKF).
“Sasa ni wakati wa Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) kufuata uamuzi wa SDT na kuteua kamati ya muda ya kuendesha shughuli za soka nchini, huku tukisubiri uchaguzi mpya kufanyika hapo baadaye.”
“Tufuateni uamuzi wa mwenyekiti wa SDT, John Ohago ambao unaenda sambamba na sheria za FIFA. Ni bora uchaguzi wa haki na ukweli ufanyike, wala sio ule utakaosimamiwa na watapeli watakaopendelea upande mmoja,” aliongeza.
Uamuzi huo kadhalika ni nafuu kwa mwenyekiti wa zamani wa FKF, Sam Nyamweya ambaye ni mpinzani mkuu wa Nick Mwendwa ambaye muda wa kamati yake kuwa mamlakani umemalizika. Nyamweya anaungwa mkono na Twaha Mbaraki anayetaka kuwa naibu wake.
Wakiufurahia uamuzi huo wa SDT, Nyamweya na Mbarak waliandamana na Ludovick Aduda pampoja na alaiyekuwa Afisa Mtendaji wa FKF, Michael Esakwa.
Kundi hilo limeupongeza uamuzi wa SDT huku likidai kwamba umeokoa soka ya Kenya kwa jumla.
“Nawapongeza mawakili na wafuasi wangu wote kwa kazi nzuri waliofanya kuhakikisha Wakenya wamepata haki,” aliongeza Nyamweya.
Kufuatia uamuzi huo wa Jumanne, Kenya inakabiliwa na hatari ya kupigwa marufuku na FIFA kushiriki katika mashindano ya kimataifa.
Katika uamuzi wake kupitia kwa video, mwenyekiti wa jopo hilo, John Ohaga alifutilia mbali uchaguzi wa mashinani uliofanyika majuzi na ule wa kitaifa uliotarajiwa kufanyika Machi 27, hii ikiwa mara ya pili hatua hiyo kuchuguliwa katika muda usiozidi miezi mitatu. Mbali na kufutilia mbali uchaguzi huo, kadhalika Ohaga alipendekeza Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) liteue tume huru ibuniwe kusimamia shughuli za FKF hadi uchaguzi mpya utakapofanyika.
Kwenye uamuzi wake, Ohaga alisema waandalizi walipuuza sheria na kanuni muhimu za uchaguzi, zoezi ambalo pia alisema liliendeshwa wakati Serikali ilikuwa imepiga marufuku shughuli zote za michezo na mikutano ya umma nchini.
Hali hii inaiweka mashakani kamati ya Nick Mwendwa ambayo muda wake wa kuwa mamlakani ulimalizika Februari 10, baada ya ule wa matawi kufika ukingoni mnamo Januari 26, hii ikimaanisha haina kundi la Mwendwa halikubaliwi kuhusika na maswala ya soka kwa sasa.
Alipokuwa nchini majuzi, mjumbe wa FIFA, Sarah Salomale aliagiza uchaguzi wa marudio ufanyika kabla ya muda wa maafisa wa sasa kumalizika, huku akisisitiza kwamba lazima bodi itakayosimamia uchaguzi izingatie maagizo na mapendekezo ya SDT.
Katika barua yake, Mwendwa alikuwa ameomba shughuli za uchaguzi zifanyike ndipo baadaye kamati yake ianze kufuata kanuni na sheria za Michezo ya 2013, ombi ambalo lilipingwa vikali ikizingatiwa kwamba amekuwa ofisini tangu 2016.
Mwendwa alikuwa amepanga uchaguzi wa kitaifa ufanyike Marchi 27, lakini jopo la Ohaga lilipata kamati ya kusimamia uchaguzi huo na makosa kadhaa, ikiwemo kupuuza sheria za uchaguzi.
FKF ililaumiwa kwa kuvuruga katiba na kuingiza vipegele vinavyoenda kinyume na matakwa ya Fifa. Kwa mfano, iligunduliwa kwamba Mwendwa alipuuza maagizo ya Msajili wa Vyama Kenya, Rose Wasike baada ya klabu na watu kadhaa kudai kwamba walikuwa wamezuiliwa kuwania vyeo.
Lakini akizungumza baada ya uamuzi huo kutolewa, Mwendwa alisema atabakia mamlakani akisubiri uamuzi wa FIFA.