Majogoo watakaowika katika fainali za AFCON
Na CHRIS ADUNGO
MWISHONI mwa wiki jana, Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) lilitoa droo ya fainali za kuwania ufalme wa Kombe la Afrika mwaka huu.
Wenyeji Misri watachuana na Zimbabwe katika mchuano wa kwanza wa fainali hizo mnamo Juni 21 jijini Cairo. Wawili hao wametiwa katika Kundi A kwa pamoja na Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wanaotarajiwa kumtegemea pakubwa mvamizi Cedric Bakambu wa kikosi cha Beijing Guoan nchini China.
Mabingwa watetezi wa taji hilo, Cameroon wametiwa katika Kundi B pamoja na Ghana, Benin na Guinea-Bissau.
Chini ya mkufunzi Clarence Seedorf, Camroon watategemeza matumaini yao ya kulihifadhi taji kwa nyota Vincent Aboubakar wa FC Porto kwa matarajio kwamba atashirikiana vilivyo na Zambo Anguisa wa Fulham.
Kwadwo Asamoah (Inter Milan), Andre Ayew (Fenerbahce), Christian Atsu (Newcastle), Thomas Partey (Atletico Madrid) na Jordan Ayew (Crystal Palace) wanatazamiwa kuwatambisha Ghana katika kundi hili.
Kocha Herve Renard wa Morocco anatarajiwa kutia kapuni ufalme wa taji la AFCON kwa mara ya tatu akidhibiti mikoba ya kikosi cha tatu tofauti. Kikosi chake cha Morocco kimetiwa katika zizi gumu na Ivory Coast, Afrika Kusini na Namibia. Mbali na Walid El Karti wa Wydad Casablanca, Morocco watategemea zaidi maarifa ya Younes Belhanda (Galatasaray) na Romain Saiss wa Wolves.
Ivory Coast walionyanyua ubingwa wa 2015, wanatazamia kutambishwa zaidi na Eric Bailly (Man-United), Wilfried Zaha (Crystal Palace) na Serge Aurier wa Tottenham Hotspur.
Madagascar na Burundi ambao ni miongoni mwa limbukeni watatu kwenye fainali hizo, wamepangwa katika Kundi B pamoja na Guinea na Nigeria watakaowategmea pakubwa huduma za Alex Iwobi (Arsenal), Ahmed Musa (Al Nassar), Kelechi Iheanacho, John Obi Mikel (Middlesbrough), Odion Ighalo (Shanghai Shenhua) na Victor Moses (Chelsea).
Kikosi kingine kinachoshiriki fainali za AFCON kwa mara ya kwanza kabisa ni Mauritania ambacho kimetiwa katika Kundi E pamoja na Mali, Angola na wenyeji wa 2004, Tunisia.
Matumaini ya kusonga kwa Guinea yatakuwa kwenye mabega wa Amadou Diawara (Napoli), Naby Keita (Liverpool) na Ibrahima Cisse wa Fulham.
Senegal, Algeria, Kenya na Tanzania ambao walifuzu kwa fainali za AFCON kwa mara ya mwisho mnamo 1980, wanakamilisha Kundi C.
Chini ya nahodha Sadio Mane, Senegal wanapigiwa upatu wa kutawala kundi hili pamoja na Algeria watakaotegemea pakubwa maarifa Nabil Bentaleb (Schalke), Islam Slimani (Leicester City), Yacine Brahimi (Porto) na Riyad Mahrez wa Man-City.
Kipenga cha kuashiria mwisho wa fainali za AFCON 2019 kimeratibiwa kupulizwa rasmi mnamo Julai 19. Ina maana kwamba wachezaji wa Afrika wanaosakata soka ya kulipwa barani Ulaya hawatakosa fursa ya kuziwajibikia klabu zao kama ilivyokuwa hapo awali.
Itakuwa mara ya kwanza kwa fainali za AFCON ambazo zimekuwa zikiandaliwa kati ya Januari na Februari hapo awali, kujumuisha vikosi 24.
Timu mbili zitakazotawala kilele cha kila kundi zitafuzu kwa hatua ya mwondoano kwa pamoja na vikosi vingine vinne vitakavyoambulia nafasi za tatu makundini ila kwa matokeo bora zaidi.
DROO YA AFCON 2019:
KUNDI A: Misri, DR Congo, Uganda, Zimbabwe
KUNDI B: Nigeria, Guinea, Madagascar, Burundi
KUNDI C: Senegal, Algeria, Kenya, Tanzania
KUNDI D: Morocco, Ivory Coast, Afrika Kusini, Namibia
KUNDI E: Tunisia, Mali, Mauritania, Angola
KUNDI F: Cameroon, Ghana, Benin, Guinea-Bissau