MALI YA BAYERN: Coutinho atua Allianz Arena kwa mkopo
Na MASHIRIKA
MUNICH, UJERUMANI
BAYERN Munich wamemsajili kiungo mvamizi Philippe Coutinho kutoka Barcelona kwa mkopo wa mwaka mmoja.
Hata hivyo, miamba hao wa soka ya Ujerumani watakuwa huru kumpokeza Coutinho mkataba wa kudumu iwapo atawaridhisha mwishoni mwa kipindi cha mkopo huo.
Kulingana na Barcelona, Bayern ambao tayari wameweka mezani kima cha Sh1 bilioni kwa minajili ya Coutinho, watalazimika kutoa Sh14 bilioni zaidi iwapo watahiari kumsajili kabisa nyota huyu mzawa wa Brazil.
Kwa mujibu wa maagano yaliyorasimisha uhamisho wa Coutinho hapo jana, Bayern watagharimia pia mshahara wa Sh1.4 bilioni ambao sosgora huyo anastahili kutia kapuni kufikia mwisho wa msimu huu.
“Uhamisho huu ni hatua kubwa kwangu. Ni hatua inayonipa jukwaa la kukabiliana na changamoto mpya katika Ligi Kuu ya nchi tofauti. Tija na fahari zaidi ni kwamba naelekea Kupiga soka katika mojawapo ya ligi bora zaidi katika soka ya bara Ulaya,” akasema Coutinho ambaye kwa sasa anasubiri kutambulishwa rasmi kwa kikosi na mashabiki wa Bayern chini ya kocha Niko Kovac.
Awali, Coutinho ambaye ameshindwa kabisa kutamba ndani ya jezi za Barcelona, alitarajiwa kuyoyomea Manchester United, Tottenham Hotspur, Arsenal, PSG au kurejea kambini mwa Liverpool. Mbali na kuyahemea maarifa ya Coutinho, Bayern wanamvizia pia chipukizi Mickael Cuisance ambaye Afisa Mkuu Mtendaji wa miamba hao wa soka ya Ujerumani Karl-Heinz Rummenigge amefichua kwamba yuko pua na mdomo kuagana na Borussia Monchengladbach.
Coutinho hakuwa sehemu ya kikosi cha Barcelona kilichozamishwa kwa 1-0 na Athletic Bilbao katika mchuano wao wa ufunguzi wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) mnamo Ijumaa iliyopita.
Nyota huyu alisajiliwa na Barcelona kutoka Liverpool mnamo Januari 2018 kwa kima cha Sh18 bilioni. Licha ya kuwafungia Barcelona mabao 21 kutokana na mechi 76, Coutinho bado hajawa kipenzi cha mashabiki ugani Camp Nou.
Makali kushuka
Kushuka kwa kiwango cha makali yake kinyume na matarajio ya mashabiki, ni suala lililowachochea Barcelona kuyawania maarifa ya fowadi Antoine Griezmann kutoka Atletico Madrid muhula huu.
Kabla ya kuafikiana na Bayern, Barcelona walikuwa radhi kumfanya Coutinho kuwa sehemu ya mpango ambao ungewawezesha kujitwalia upya huduma za Neymar Jr baada ya kuweka mezani kima cha Sh11 bilioni vilevile.
Kwa mujibu wa gazeti la Sport nchini Uhispania, ni fahari tele kwa Coutinho kubanduka kambini mwa Barcelona hasa ikizingatiwa kwamba tumaini lake la kuunga kikosi cha kwanza limedidimizwa zaidi baada ya ujio wa Griezmann ambaye anatarajiwa kushirikiana zaidi na Lionel Messi, Luis Suarez na Neymar anayetarajiwa kwa sasa kukamilisha safu ya mbele ya miamba hao wa soka ya Uhispania.
Mkuu wa masuala ya soka uwanjani Emirates, Raul Sanllehi alitazamiwa kufanikisha uhamisho huo wa Coutinho licha ya Arsenal kutokuwa radhi kufungulia mifereji yao ya fedha.
Ilivyo, kocha Unai Emery amekuwa akisisitiza kwamba alipokezwa kima cha Sh5.9 bilioni pekee kwa minajili ya kusajili wachezaji wapya msimu huu.