Michezo

MALI YA BRUGGE: Wanyama aondoka Tottenham Hotspur

August 31st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

VICTOR Mugubi Wanyama ameondoka Tottenham Hotspur na kujiunga na Club Brugge nchini Ubelgiji, ripoti zimesema.

Kiungo huyu mkabaji aliyesherehekea kufikisha umri wa miaka 28 mnamo Juni 25, aliungana na kocha wake wa zamani Mauricio Pochettino kutoka Southampton mwaka 2016 kwa kandarasi ya miaka mitano iliyotarajiwa kukatika Juni 30 mwaka 2021.

Hata hivyo, Wanyama ametatizika kuwa tegemeo katika kikosi cha kwanza kutokana na majeraha, na kuwasili kwa Tanguy N’dombele na Giovani Lo Celso kumefanya mambo yawe magumu hata zaidi.

Kwa hivyo, Wanyama ametafuta kibarua kipya nchini Ubelgiji kuichezea Brugge ambayo inaaminika ilikubaliana na Tottenham ada ya uhamisho ya Sh1.2 bilioni.

Ada hii inaweza kupanda hadi Sh1.6 bilioni kutegemea mchango wa Wanyama katika klabu ya Brugge, ambayo ripoti zinasema italipa Sh1.1 bilioni kwanza na kisha nyongeza ya Sh567.2 milioni akiifanyia kazi nzuri.

Wanyama si mchezaji wa kwanza kujiunga na Brugge kutoka Ligi Kuu ya Uingereza katika kipindi hiki kirefu cha uhamisho. Kipa wa Liverpool, Simon Mignolet alitua Brugge mapema mwezi huu.

Sawa na Spurs, Brugge pia itashiriki Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huwa wa 2019-2020.

Hata hivyo, Brugge ina kibarua kigumu kufika raundi ya 16-bora katika Kundi A linalojumuisha Paris Saint-Germain, Real Madrid na Galatasaray, ambayo pia iliwahi kuhusishwa na Wanyama mapema mwezi huu.

Wanyama anaondoka Spurs baada ya kuichezea mechi 36 (msimu 2016-2017), 18 (2017-2018) na 13 (2018-2019) kwenye Ligi Kuu, ingawa hakupatiwa hata sekunde moja msimu huu.

Hakutumiwa katika mechi ya ligi ya kufungua msimu dhidi ya Aston Villa, ambayo Spurs ilishinda 3-1. Aliachwa nje kabisa dhidi ya Manchester City iliyotamatika 2-2 na kichapo cha 1-0 kutoka kwa Newcastle United.

Jumla ya mechi 93

Kwa jumla, Wanyama alichezea Spurs mechi 93 katika mashindano yote na kuifungia mabao sita ikiwemo ‘roketi’ moja ambayo mashabiki wa Spurs hawatawahi kuisahau dhidi ya Liverpool msimu uliopita.

Nahodha huyu wa Kenya alipokea mshahara wa Sh8.2 milioni kila wiki akiwa Spurs.

Mapema juma hili, ripoti zilidai kuwa amekubali mshahara uliopunguzwa hadi Sh6.3 milioni kila wiki ili kufanikisha uhamisho wake hadi Brugge.

Katika klabu ya Brugge, ambayo itaalika mabingwa watetezi Genk mnamo kesho Jumapili ligini, Wanyama ataungana na kocha Philippe Clement, 45.

Wanyama na Clement walicheza pamoja katika klabu ya Beerschot nchini Ubelgiji alikoanzia Mkenya huyo soka yake ya malipo msimu 2009-2010. Ingawa bado uhamisho wa Wanyama haujatangazwa rasmi, anaaminika kutoka nchini Uingereza akiwa na uraia wa nchi hiyo baada ya kusakata humo tangu msimu 2013-2014.