Michezo

MALI YA WATFORD: Danny Welbeck

August 20th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na MWANGI MUIRURI

HUKU mashabiki wa Arsenal wakishabikia fomu yao kwa sasa ambapo katika mechi mbili za ufunguzi wa msimu mpya wana pointi sita, kwa upande mwingine wamenuna baada ya Daniel Nii Tackie Mensah Welbeck ‘Danny Welbeck’ kujiunga na klabu ya Watford inayoshiriki ligi hiyo kuu ya Uingereza (EPL).

Arsenal ya Unai Emery ilifungua msimu kwa kuikanyaga Newcastle 1-0 na wikendi jana wakaiadhibu Burnley 2-1.

Turejee kwa Danny. Ni mwana wa Victor Welbeck na Elizabeth Welbeck. Ana ndugu mmoja kwa jina Chris Welbeck na kwa kweli ni msiri katika

maisha yake na pengine ndiyo sababu hana kashfa za kimapenzi ambazo zimemulikwa na vyombo vya habari na pia hana mke ambaye anajulikana rasmi.

Hata hivyo, ameorodheshwa kama miongoni mwa wanaopenda kutazama filamu, kuogelea na kucheza kandanda.

Mzawa huyu wa mji wa Manchester na ambapo alizaliwa Novemba 26, 1990, amekuwa kipenzi cha wengi ambao hupendezwa na juhudi zake ugani na bidii za mchwa katika kuvizia mabeki na kasi kamili ya kuwazunguka na kutinga magoli.

Lakini kufuatia jinamizi lake la kuandamwa na majeraha, baada ya kuwa ugani Emirates kwa kipindi cha miaka mitano, aliruhusiwa hatimaye kuondoka bila gharama yoyote na ambapo alitua katika kambi ya wapinzani hao Watford.

Welbeck alianza kukolea ueledi wake wa usakataji soka katika taasisi ya makinda wa Manchester United na ambapo alijiunga na timu ya Kwanza

ikifahamika kama Red Devils mwaka wa 2008. Alikuwa amesajiliwa na Alex Ferguson ndani ya akademia ya Man U akiwa na miaka saba pekee.

Alitumwa hadi Klabu ya Preston North End mwaka wa 2009 na hatimaye katika klabu ya Sunderland ambapo alihudumu msimu wa 2010/11 na ambapo katika msimu wa 2014/15 aliuzwa hadi Arsenal kwa kima cha Euro 16 milioni.

Alikuwa ameorodheshwa kama mchezaji wa timu ya kwanza na taifa lake la Uingereza mwaka wa 2011 na ambapo mechi ya kwanza akiwajibikia uzalendo wa utaifa, akawa katika timu ambayo ilitoka sare na taifa la Ghana katika mechi ya kirafiki.

Wazazi wake ni raia wa taifa hilo la Ghana.

Alitikisa nyavu kwa mara yake ya kwanza na la ushindi mnamo Juni 2, 2012, katika mechi ya kirafiki kati ya Uingereza na taifa la Ubelgiji na Welbeck akawa sasa amekomaa na ambapo amekuwa akionekana ugani mara si haba na akisisimua hisia na bongo kupitia usogora wake.

Kwa mashabiki sugu wa Arsenal nchini Kenya, alikuwa amepewa jina la majazi la “Kioko” kufuatia mapenzi yake ya kunyolewa mtindo wa boksi na ambao sanasana huenziwa sana na wazawa wa jamii hiyo ya Mashariki mwa Kenya.

Mnamo Septemba 2, 2014, Welbeck alitemwa na mkufunzi Louis van Gaal akimsema kuwa hakuwa na tajiriba na mashiko ya ubora na ndipo akatolewa kafara ndio sogora Falcao atue ugani Old Trafford. Alikuwa amechezea Manchester United mara 142 akitikisa nyavu mara 29.

Welbeck alicheza mechi yake ya kwanza akiwa na jezi ya Arsenal dhidi ya Manchester City mnamo Septemba 13 na ambapo walitoka sare ya 2-2 na licha ya utepetevu wake ugani, aliyekuwa mkufunzi wa Arsenal, Arsene Wenger akaomba mashabiki waqwe na subira na kiungo huyo mshambulizi ambaye hutumia guu la kulia.

Na akatikisa nyavu akicheza dhidi ya Aston Villa mnamo Septemba 20 katika ushindi wa 3-0 na akasaidia Mesut Ozil kutikisa nyavu katika suhindi huo na ndipo imani ya Wenger kwake ikawa na taswira ya uhakika.

Oktoba 1 alitikisa nyavu mara tatu katika mechi ya Champions League dhidi ya Galatasaray na ambapo Arsenal iliibuka kidedea kwa magoli 4-1.

Machi 9, 2015, Welbeck alitikisa nyavu katika ushindi dhidi ya Manchester United na goli ambalo lilitupa nje klabu hiyo yake ya zamani katika michuano ya kombe la FA, msumari juu ya kidonda ikiwa ni kwamba alitinga goli hilo ugani Old Trafford. Mwezi uliofuata, alijipata mkekani akiuguza jeraha na pia akakosa kufungua msimu wa 2015/16 ambapo alikaa nje ya uga hadi Februari 2016.

Alirejea ugani kusakata soka mnamo Februari 14, 2016, na ambapo alichangia pakubwa ukomavu wa kikosi cha Arsenal.

Licha ya kuandamwa na majeraha ya mara kwa mara, amejizatiti na kubakia wima akiwa na afueni ya uzima wake kiafya ugani, hali ambayo humpa imani ya mashabiki.

Taharuki ni kwamba amekuwa akichezea Arsenal na kwa kawaida, ni lazima awe anafahamu vyema mbinu na njama zao kiasi kwamba wakati ataingia ugani kumenyana nao akiwajibikia Watford, anaweza akawapa mashabiki wake wa zamani kilio cha nyavu.