Man City yabomoa ubora wa mabao wa Arsenal ikibakisha 2 pekee
Na MWANGI MUIRURI
KLABU ya Manchester City sasa inaonekana kuwa imesuka njama ya kuibandua Arsenal kutoka kwa ubabe wa ubora wa magoli katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).
Hadi sasa, Arsenal ina ubora wa magoli 60 nayo Man City ikiwa na 58 huku Liverpool ikiwa ya tatu baada ya kujipa ubora wa 43.
Hali hii ni hatari kwa Arsenal ambayo ilikuwa inategemea kutumia ubora huo wa magoli kama njia mojawapo ya kujipa ubingwa wa EPL msimu huu.
Hata hivyo, baada ya kujivunia kuwa juu ya jedwali na pia kuwa na magoli mengi, matumaini ya Arsenal yalikuwa kwamba kinyang’anyiro kingeishia kuwa cha kuamuliwa na ubora wa magoli, basi ingepata afueni.
Kila timu ikiwa na nafasi ya kujizolea pointi sita katika mechi mbili za mwisho, Man City ni ya kwanza kwa msimamo wa Ligi ikiwa na pointi 85, Arsenal ya pili kwa pointi 83 huku Liverpool ikiwa na pointi 78.
Bila shaka mambo yalivyo sasa, matumaini ya Liverpool kujipa ubingwa ni sawa na kumkama kuku ukisaka maziwa.
Nayo Arsenal inang’ang’ana kwa unono wa ngozi ya jino kwamba kuna mkosi wa kulemaza City walio mbele ndio iilalie bahati hiyo mlango wazi.
“Lakini hawa ‘wanyama’ wa Man City wamechukulia hii ligi kama ya kuaibisha Arsenal. City imekuwa ikitwanga wapinzani kwa ukali unaokaa uhasama. Hali kwa sasa ni kwamba katika mechi mbili ambazo zimesalia kwa kila timu hizi tatu, Man City itakuwa imeibandua Arsenal kutoka kidedea kwa kigezo cha magoli,” akasema Dkt Waweru Mungai ambaye ni shabiki wa Arsenal.
Dkt Mungai anafanya kazi katika Wizara ya Afya nchini Kenya.