MAN CITY YAPONEA: Timu kuendelea kusajili wachezaji
Na MASHIRIKA
MANCHESTER City wameponea kupigwa marufuku ya usajili wachezaji baada ya kukubali walivunja sheria za kusaini wachezaji chipukizi za Shirikisho la Soka Duniani (Fifa).
Hata hivyo, mabingwa hawa wa Ligi Kuu ya Uingereza hawajaepuka faini ya Sh39.2 milioni.
Baada ya kukamilisha uchunguzi wake dhidi ya City, Fifa ilisema Jumanne kuwa klabu hii ilivunja kifungu cha 19 cha sheria zake ambacho kinasema, “Uhamisho wa wachezaji kutoka nchi ya kigeni unaruhusiwa tu kama mchezaji amepitisha umri wa miaka 18.”
City inasema kuwa ukiukaji huo wa sheria, ambao wote ulifanyika kabla ya Desemba mwaka 2016, ulitokana na “kutoelewa kanuni zinazozungumziwa.”
Mabingwa wa zamani wa Uingereza Chelsea walipigwa marufuku kusaini wachezaji kwa vipindi viwili vya uhamisho kwa kosa sawa na la City, lakini imekata rufaa ikitaka adhabu hiyo iondolewe.
City ilisema kuwa kosa lake lilihusu wachezaji waliokuwa wakifanyiwa majaribio na kuchezeshwa kwao katika mechi za kirafiki, na kuwa klabu hiyo “imekuwa ikifuata sheria tangu wakati huo.” Klabu ya City pia iliongeza kuwa “ilishirikiana kikamilifu” na Fifa katika uchunguzi dhidi yake.
“Klabu hii inakubali makosa ya kuvunja sheria zinazozungumziwa yaliyotokana na kuzielewa kivingine,” ilisema City.
Mwaka 2018 wachezaji wawili kutoka akademia ya soka ya Right to Dream nchini Ghana – George Davies kutoka Sierra Leone na raia wa Ghana, Dominic Oduro – waliambia gazeti la Jyllands-Posten nchini Denmark kuwa walisajiliwa na City na kuichezea mechi kadhaa kabla wafikishe umri wa miaka 18.
“Kamati ya Nidhamu ya Fifa imeadhibu klabu ya Uingereza ya Manchester City FC kwa uvunjaji wa sheria zinazohusu uhamisho wa wachezaji kutoka nje ya Uingereza na kusajili wachezaji walio chini ya umri wa miaka 18,” wasimamizi hao wa soka duniani walisema katika taarifa yao.
“Manchester City FC ilipatikana na hatia ya kuvunja sheria, miongoni mwa makosa mengine, katika kifungu cha 19 cha sheria za Fifa kuhusu hali ya wachezaji na uhamisho wao.
“Kamati ya nidhamu ilifikia uamuzi huo wa kupiga klabu hii faini ya Sh39.2 milioni ikitilia maanani kuwa City ilikuwa imekubali kufanya makosa.”
Chelsea iliadhibiwa na Fifa mwezi Februari kwa kukiuka sheria kuhusu wachezaji 29 chipukizi, na kupigwa faini ya Sh57.2 milioni mbali na kupokea marufuku ya kutosajili wachezaji kwa vipindi viwili.
Kukata rufaa
Mwezi Juni, Chelsea, ambayo haikuruhusiwa kununua mchezaji katika kipindi kirefu cha uhamisho kilichotamatika Agosti 9, ilitangaza kuwa itawasilisha rufaa yake katika Mahakama ya Kusikiza kesi za michezo (CAS) baada ya Fifa kukataa rufaa yake ya kwanza.
Mei 2017 City ilipigwa marufuku kusajili wachezaji kutoka akademia kwa miaka miwili na kutozwa faini ya Sh37.3 milioni baada ya kuvunja sheria za uhamisho wa wachezaji za Ligi Kuu ya Uingereza.
City bado inachunguzwa na Shirikisho la Soka barani Ulaya (Uefa) kwa madai mengine ya kuvunja sheria zinazosema klabu haifai kutumia fedha zaidi ya mapato yake (FFP).