• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:55 AM
Man U wawanie huduma za Allegri kabla ya Chelsea, PSG, Bayern kubisha

Man U wawanie huduma za Allegri kabla ya Chelsea, PSG, Bayern kubisha

NA CHRIS ADUNGO

BAADA ya Juventus kumfuta kazi kocha Massimiliano Allegri mwishoni mwa wiki jana, beki wa zamani wa Liverpool Steve Nicol aliwapendekezea Manchester United kumtimua Ole Gunnar Solskjaer na kuwania upesi huduma za Allegri.

Kulingana na Nicol, hakuna mjadala wowote unaostahili kuibuka lijapo suala la kulinganisha ubora wa Allegri na Solskjaer. Kwa kiasi kikubwa, naunga mkono pendekezo la Nicol – kwamba iwapo Man-United wanafikiria kurejesha kumbukumbu za miaka ya awali walipokuwa miamba wa soka ya Uingereza – basi Allegri ndiyo dawa mujarabu.

Ingawa kumtimua Solskjaer kutawasawiri wasimamizi wa kikosi cha Man-United kuwa binadamu wasio na utu, nitaomba pia shabiki wa kikosi hiki kulizamia suala hili vilivyo na kuliwazia kabisa kwa kina. Je, ni nani ungependelea awe kocha wa kikosi chako kati ya Allegri na Solskjaer? Bilas haka ni Solskjaer, na hilo halina ubishi.

Tangu wamfute kazi kocha Antonio Conte na kumwajiri Allegri mnamo 2014, Juventus wamekuwa wakitia kapuni ubingwa wa taji la Serie A kila mwaka huku wakitinga pia fainali ya UEFA mara mbili.

Hadi kufutwa kazi, Allegri aliwahi kuanika azma yake ya kudhibiti mikoba ya kikosi kinachoshiriki soka ya EPL. Hata hivyo, alidokeza huenda akalazimika kupumzika kidogo kabla ya kutafuta hifadhi mpya.

Licha ya Man-United kuimarika pakubwa katika hatua za mwanzo za ukufunzi wa Solskjaer, miamba hao wa soka ya Unigereza waliporomoka ghafla katika wiki chache za mwisho za kampeni za EPL na hivyo kuambulia nafasi ya sita jedwalini.

Baada ya kutia saini mktaba wa kudumu uwanjani Old Trafford na kusitisha mipango ya Man-United ya kutafuta mkufunzi mwingine, Solskjaer aliwaongoza vijana wake kusajili ushindi mara mbili pekee kutokana na michuano 10 ya mwisho wa msimu.

Japo Juventus walianza msimu wakiwa na malengo ya kutia kapuni jumla ya mataji manne ya UEFA, Serie A, Coppa Italia na Italian Super Cup; mawili kati ya maazimio hayo yaliwezekana.

Super Cup ni taji la kwanza kwa Juventus kujitwalia baada ya kuongozwa na sajili mpya Cristiano Ronaldo kuwapepeta AC Milan jijini Jeddah mnamo Januari.

Ubingwa wa Serie A ambalo Juventus walilinyanyua kwa mara ya nane mfululizo ni taji la pili kwa kikosi hicho kutia kibindoni. Hakuna klabu yoyote katika historia ya Ligi Kuu tano za bara Ulaya imewahi kuufikia ufanisi huo.

Kingine ambacho huenda kilichangia kufutwa kwa Allegri ni maamuzi yake ya kuchezesha wavamizi watatu katika mfumo wa 4-3-3 uliomsaza nje wachezaji Douglas Costa na Paulo Dybala aliyewahi kupigiwa upatu kuwa mrithi wa nyota Lionel Messi katika soka ya Argentina.

Dybala ambaye pia amewahi kuwachezea Palermo, alifunga jumla ya mabao matatu mnano 2017 na kuwasaidia waajiri wake kuwazima Barcelona 3-0 katika mchuano wa mkondo wa kwanza wa robo-fainali za UEFA.

Kubwa zaidi lililomfuta Allegri kambini mwa Juventus ni maamuzi yake ya kushawishi usimamizi kumsajili Ronaldo kwa matumaini kwamba angaliwasaidia kutia kibindoni ufalme wa UEFA. Hili halikutimia.

Kutua kwa nyota Ronaldo kambini mwa Juventus kulitarajiwa kuamsha msisimko mpya miongoni mwa mashabiki wa soka ya Italia huku macho yakielekezwa kwa fowadi huyo mzawa wa Ureno.

Akiwa miongoni mwa watu maarufu zaidi duniani, Ronaldo anajivunia zaidi ya wafuasi 310 milioni katika mitandao yote ya kijamii. Hili lilitazamiwa kufanya Serie A na hususan Juventus, kuwa kivutio kikubwa cha mashabiki.

Hatua ya Ronaldo kutua Italia ilitazamiwa kurejesha hadhi ya soka ya taifa hilo ambalo liliwahi kutoa wanafainali wawili wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2003 – Juventus na AC Milan. Mbali na kuchangia kuongezeka kwa idadi ya mashabiki wa Juventus, Ronaldo alikuwa awavunie waajiri wake faida tele kutokana na wingi wa tiketi za kuuzwa katika kila mchuano. Hili nalo halikutimia muhula huu.

You can share this post!

Milner mtemi wa soka ambaye ana hela mithili ya changarawe

Lingard ni kichekesho kingine pale Old Trafford

adminleo