MAN-UTD MAWINDONI: Wenyeji wa Old Trafford kukabiliana na Partizan Belgrade
Na MASHIRIKA
MANCHESTER, Uingereza
MANCHESTER United watakuwa nyumbani ugani Old Trafford kukabiliana na Partizan Belgrade ya Serbia katika pambano la Europa League, Kundi L.
Manchester waliibuka na ushindi wa 1-0 ugenini katika mkondo wa kwanza ambapo ushindi utawawezesha kufuzu kwa hatua ya maondoano.
Marcus Rashford, Victor Lindelof na Harry Maguire waliokuwa kikosini mwishoni mwa wiki dhidi ya Bournemouth wanatarajiwa kuanza tena mechi ya leo.
Kumekuwa na madai kwamba huenda wakapumzishwa kutokana na majeraha madogo waliopata kwenye mechi ya Carabao Cup dhidi ya Chelsea.
Lakini kiungo Paul Pogba anatarajiwa kusalia nje hadi mwezi Disemba kutokana na jeraha la goti, pamoja na Luke Shaw, Nemanja Matic na Axel Tuanzebe wanaosumbuliwa na majeraha mbalimbali.
Kadhalika, Diogo Dalot ataikosa mechi ya leo kutokana na jeraha pamoja na Eric Bailly na Timothy Fosu-Mensah.
Kocha Ole Gunnar Solskjaer amelazimika kufanya mabadiliko ya mara kwa mara msimu huu kutokana na majeraha kwa mastaa wake kadhaa, na huenda akafanya hivyo leo.
Vijana hao wanaongoza jedwalini baada ya kuendeleza rekodi ya kutoshindwa katika mechi tatu, wala kufungwa bao lolote katika mechi hizo.
Rekodi nzuri
Kadhalika wanajivunia rekodi nzuri ya kutoshindwa nyumbani katika mashindano tofauti msimu huu, baada ya kushindwa mara moja pekee ugani Old Trafford.
Partizan wanakamata nafasi ya tatau jedwalini baada ya sare ya 2-2 dhidi ya AZ Alkmaar kwenye mechi ya utangulizi, na ushindi wa 2-1 dhidi ya Astana na kushindwa mara moja na Manchester United.
Kwa sasa, wamo katika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu ya Serbia, baada ya ushindi mara nne, sare mbili na kushindwa mara tatu katika mechi 14.
Partizan ni klabu nambari mbili kwa ukubwa nchini Serbia, baada ya Red Star.
Wameshinda mataji 27 ya kitaifa, yakiwemo 11 ya Ligi Kuu ya Yugoslavia, manane ya Ligi Kuu ya Serbia & Montenegro na manane ya Ligi Kuu ya Serbia.
Ndiyo klabu ya kwanza kutoka Ulaya Mashariki kutinga fainali ya Ulaya, baada ya kufanya hivyo mnamo 1966, na hii itakuwa mara yao ya 44 kushiriki katika michuano hii, mbali na kutoa wachezaji kadhaa waliochezea Manchester United miaka ya hapo awali.