Manangoi aomba Wakenya msamaha baada ya kupigwa marufuku
Na CHRIS ADUNGO
MTIMKAJI Elijah Manangoi aliyeibuka bingwa wa Afrika katika mbio za mita 1,500 barani Afrika mnamo 2018, amewaomba Wakenya na wadau wa riadha msamaha na kukiri kwamba atawajibikia matendo yake ya kukosa kujiwasilisha kwa vipimo vya pufya baada ya kupigwa marufuku.
Manangoi aliyeibuka bingwa wa dunia katika mbio za mita 1,500 mnamo 2017 jijini London, Uingereza, alipigwa marufuku ya miaka miwili na Kitengo cha Maadili (AIU) cha Shirikisho la Riadha Duniani (WA) mnamo Novemba 13, 2020.
“Nimekubali maamuzi ya AIU dhidi yangu japo ni magumu na mazito sana. Naomba radhi kwa kuiangusha nchi yangu, Shirikisho la Riadha la Kenya (AK), usimamizi wangu, kocha wangu na wote ambao wamekuwa na imani kubwa kwangu tangu nijitose katika ulingo wa riadha,” akasema Manangoi kwenye mtandao wake wa Facebook.
Manangoi hata hivyo ameahidi makuu na kusisitiza kwamba atarejea ulingoni kwa matao ya juu zaidi pindi baada ya marufuku yake kukamilika mnamo Disemba 21, 2021.
“Mimi ni mwanariadha anayependa kushinda mapambano ya mbio bila kutumia njia za mkato. Nitarejea hivi karibuni,” akasema kwa kuwataka wanariadha wengine kuwa waangalifu sana kuhusiana na kanuni ya AIU ya kutojiwasilisha kambini mwa vipimo vya dawa za kusisimua misuli.
“Ni kanuni rahisi lakini kosa dogo tu la kutojiwasilisha linaweza likakuathiri na kuzamisha kabisa taaluma ya mtu. Ni aibu kubwa,” akaonya Manangoi.
Manangoi alipigwa marufuku baada ya kukosa kujiwasilisha mara tatu kwa vipimo vya pufya mnamo Julai 3, Novemba 12 na Disemba 22, 2019.
Kwa mujibu wa kanuni mpya za AIU, mwanariadha anayefanyiwa vipimo vya pufya ghafla, anatarajiwa kujiwasilisha kambini mwake mwa mazoezi chini ya dakika 60 kila anapoombwa kufanya hivyo na maafisa wa WA.
Kwa Manangoi, mwanariadha huyo hakujiwasilisha katika kambi yake ya mazoezi ya Rongai Nazarene alipotakiwa kufanya hivyo na maafisa wa AIU katika tarehe hizo kati ya saa mbili na saa tatu usiku.
Matokeo yote yaliyosajiliwa na Manangoi kuanzia Disemba 22, 2019 sasa yamefutiliwa mbali huku akipoteza pia medali, mataji, fedha za kushiriki mbio na tuzo zote nyinginezo alizojinyakulia baada ya kipindi hicho.
Manangoi, 27, alikuwa miongoni mwa wanariadha wanne wa Kenya ambao waliadhibiwa AIU mnamo Julai 2020 kwa kukiuka kanuni zinazodhibiti matumizi ya pufya.
Watatu wengine ambao wamepigwa marufuku ni Patrick Siele, Kenneth Kiprop Kipkemoi na Mercy Jerotich Kibarus ambao ni watimkaji wa marathon.
Baada ya kuibuka mfalme wa dunia mnamo 2017, Manangoi alitawala Michezo ya Jumuiya ya Madola na mbio za Bara la Afrika mnamo 2018. Anajivunia pia kushinda mbio za mita 1,500 kwenye duru mbalimbali za Wanda Diamond League katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Kwa mujibu wa kanuni za Shirika la Kukabiliana na Pufya Duniani (WADA), mwanariadha anayekosa kufanyiwa vipimo mara tatu chini ya kipindi cha miezi 12, hupigwa marufuku moja kwa moja.
Siele, 24, alisimamishwa kwa muda kwa kosa la kukwepa na (au) kutojiwasilisha kwa minajili ya vipimo vya afya mara tatu mfululizo. Muda wake bora zaidi katika mbio za marathon ni saa 2:10:42 aliouandikisha katika Shanghai International Marathon mnamo 2019. Aliambulia nafasi ya sita katika mbio hizo.
Huku Manangoi na Siele wakisimamishwa kwa muda kwenye ulingo wa riadha wakati huo, Kipkemoi na Kibarus walipigwa marufuku ya vipindi virefu baada ya chembechembe za dawa haramu aina ya Terbutaline na Norandrosterone kupatikana katika sampuli zao za damu.
Kipkemoi sasa atakuwa nje ya ulingo wa riadha kwa miaka miwili huku marufuku yake yakianza kutekelezwa rasmi mnamo Februari 25, 2020. Matokeo yote katika mbio alizozishiriki tangu Septemba 12, 2019 pia yalifutiliwa mbali.
Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 35 aliambulia nafasi ya pili kwenye Michezo ya Afrika mnamo 2011 nchini Msumbuji kabla ya kuibuka mshindi wa NN Rotterdam Marathon nchini Uholanzi mnamo 2018. Alikamilisha mbio za mita 10,000 kwenye Riadha za Dunia zilizoandaliwa jijini London, Uingereza mnamo 2017.
Kwa upande wake, Kibarus, 36, alipigwa marufuku ya miaka minane ambayo yaanza kutekelezwa rasmi mnamo Disemba 5, 2019. Matokeo yote ya mbio alizonogesha tangu Septemba 13, 2019 yalifutiliwa mbali. Kibarus aliibuka mshindi wa Sydney Marathon mnamo 2018.