• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 1:20 PM
Manchester City wafalme wa Carabao

Manchester City wafalme wa Carabao

Na MASHIRIKA
MANCHESTER City waliweka hai matumaini ya kutia kapuni jumla ya mataji manne msimu huu baada ya kupepeta Chelsea 4-3 wikendi jana katika fainali ya Carabao Cup.
Man-City wanafukuzia pia ufalme wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na Kombe la FA hadi kufikia sasa muhula huu.
Chini ya kocha Pep Guardiola, miamba hao wa soka ya Uingereza walitawazwa wafalme wa Carabao (League Cup)baada ya kuchabanga Chelsea ugani Wembley.
Mshindi wa mechi hiyo aliamuliwa kupitia mikwaju ya penalti baada ya pande zote kuambulia sare tasa mwishoni mwa dakika 120.
Ingawa hivyo, kitakachokumbukwa zaidi katika fainali hiyo ni ukaidi wa kipa Kepa Arrizabalaga ambaye alikataa kuondoka uwanjani licha ya kocha Maurizio Sarri kutaka ampishe mlinda-lango Willy Caballero.
Kepa ambaye ni mzawa wa Uhispania, alisajiliwa na Chelsea kwa kima cha Sh9.2 bilioni kutoka Athletic Bilbao ya Uhispania mwanzoni mwa msimu huu.
Alimkaidi Sarri aliyepania kumwajibisha Caballero aliyedaka penalti tatu mnamo 2016 na kuwasaidia waliokuwa waajiri wake Man-City kunyanyua ubingwa wa Carabao Cup baada ya kuwazidi nguvu Liverpool kwenye fainali.
Raheem Sterling aliwafungia Man-City penalti ya ushindi baada ya Kepa kuunyaka awali mkwaju wa winga Leroy Sane. Mabao mengine ya Man-City yalifungwa na wachezaji Ilkay Gundogan, Sergio Aguero na Bernardo Silva.
Penalti ya kiungo Jorginho aliyesajiliwa na Chelsea mwishoni mwa msimu jana, ilinyakwa na kipa Ederson Moraes huku beki David Luiz akishuhudia mkwaju wake ukibusu mlingoti wa lango la wapinzani wao.
Cesar Azplicueta, Emerson na Eden Hazard ni wachezaji wa Chelsea waliofunga penalti zao.
Cheche
Ukaidi wa Kepa ulimsaza Sarri katika ulazima wa kurushiana cheche za maneno na sehemu ya usimamizi wa benchi la kiufundi huku kocha huyo mzawa wa Italia akionekana kwa wakati fulani kutaka kuondoka uwanjani kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mchezo kupulizwa.
Ushindi wa Man-City unafikisha jumla ya mataji ya Carabao Cup kabatini mwao kufikia sita, mawili zaidi kuliko Liverpool ambao kwa sasa wanaongoza kilele cha jedwali la EPL licha ya kuambulia sare tasa dhidi ya Man-United ugani Old Trafford.
Hii ni mara ya pili kwa Man-City kutia kapuni ufalme wa League Cup kupitia penalti baada ya kuwapiku Liverpool mnamo 2016.
Aidha, ni fainali ya kwanza tangu 2009 kuwahi kumalizika kwa sare tasa ambapo Man-United waliwapepeta Tottenham kupitia penalti.

You can share this post!

KCB kufadhili mafunzo ya makocha wa voliboli

Rodgers, Moyes wako pazuri zaidi kupokezwa ukocha Leicester...

adminleo