Manchester City wapewa Real Madrid katika robo-fainali Uefa
Na GEOFFREY ANENE
MABINGWA watetezi Manchester City watakutana na washikilizi wa rekodi ya mataji mengi (14) Real Madrid baada ya droo ya robo-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya msimu 2023-2024 kufanywa Ijumaa.
Wanafainali wa msimu 2005-2006 Arsenal watalimana na mabingwa mara sita Bayern Munich walioshinda taji mara ya mwisho mwaka 2020.
Paris Saint-Germain (PSG) wanaojivunia mfumaji matata Kylian Mbappe hawajawahi kutwaa taji la Klabu Bingwa Ulaya. Walichapwa na Bayern katika fainali ya mwaka 2020. Watapepetana na Barcelona walionyakua taji lao la tano na mwisho la Klabu Bingwa Ulaya mwaka 2015.
Atletico, ambao matokeo yao mazuri ya Klabu Bingwa Ulaya ni nafasi ya pili mwaka 1974, 2014 na 2016 watakabana koo na washindi wa 1997 Borussia Dortmund.
Mechi za robo-fainali ni kati ya Aprili 9 na Aprili 17, nusu-fainali ni kati ya Aprili 30 na Mei 8, nayo fainali ni ugani Wembley jijini London mnamo Juni.
Mshindi wa Arsenal/Bayern atakutana na Real Madrid/Manchester City katika nusu-fainali nayo nusu-fainali nyingine itakutanisha Atletico Madrid/Dortmund na PSG/Barcelona.