Manchester City washinda Olympiakos 1-0
Na MASHIRIKA
KOCHA Pep Guardiola amesisitiza kwamba mabao “yatajileta yenyewe” baada ya Manchester City kufunga goli moja pekee dhidi ya Olympiakos licha ya kutamalaki mchezo na kumiliki asilimia kubwa ya mpira katika gozi la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Novemba 25, 2020 nchini Ugiriki.
Ushindi wa Man-City katika mchuano huo uliwakatia tiketi ya hatua ya 16-bora ya UEFA huku wakisalia na mechi mbili zaidi za kutandaza katika Kundi C.
Masogora wa Guardiola walijibwaga ugani dhidi ya Olympiakos wakihitaji alama moja pekee ili kujipa uhakika wa kusonga mbele katika kampeni za UEFA.
Bao la pekee na la ushindi kwa upande wa Man-City waliowaelekezea Olympiakos jumla ya fataki 25, lilifungwa na chipukizi raia wa Uingereza, Phil Foden katika dakika ya 36.
Licha ya kuchezea katika uwanja wa nyumbani, Olympiakos walishindwa kuelekeza kombora lolote langoni mwa wageni wao hadi dakika ya 88. Hata hivyo, jaribio lao hilo lilidhibitiwa vilivyo na kiungo Ilkay Gundogan aliyeshirikiana vilivyo na Bernardo Silva.
Kiungo Kevin de Bruyne aliachwa nje ya kikosi cha Man-City kilichomkaribisha tena fowadi Sergio Aguero kwa dakika 13 za mwisho wa kipindi cha pili baada ya kupona jeraha la goti.
Ni matarajio ya Guardiola kwamba ushindi waliouvuna dhidi ya Olympiakos utawapa motisha zaidi kutamba katika jumla ya michuano 11 ijayo kabla ya kampeni za mwaka huu wa 2020 kukamilika rasmi.
Man-City walijibwaga ugani kwa minajili ya mechi dhidi ya Olympiakos wakipania kujinyanyua baada ya kupokezwa kichapo cha 2-0 na Tottenham Hotspur katika mchuano wa awali wa EPL mnamo Novemba 21, 2020.
Man-City ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya 13 kwenye jedwali la EPL kwa alama nane zaidi nyuma ya viongoziu Tottenham, wanashuhudia mwanzo mbaya zaidi ligini tangu 2008.
Kikosi hicho kilichotwaa ufalme wa EPL mnamo 2017-18 na 2018-19, hakijafunga zaidi ya bao moja katika EPL tangu wapokezwe kichapo cha 5-2 na Leicester City mnamo Septemba 2020.
Man-City kwa sasa wanajiandaa kuwa wenyeji wa Burnley katika EPL mnamo Novemba 28 kabla ya kuwaendea FC Porto ya Ureno kwa gozi la UEFA mnamo Disemba 1, 2020.