Manchester City ya wanawake yamteua Gareth Taylor awe kocha wao
Na CHRIS ADUNGO
KIKOSI cha soka ya wanawake cha Manchester City kimemteua mshambuliaji matata wa zamani wa timu ya taifa ya Wales, Gareth Taylor kuwa kocha mpya kwa mkataba wa miaka mitatu.
Taylor, 47, aliwahi kuvalia jezi za Man-City kati ya 1998 na 2001. Hadi kuteuliwa kwake, alikuwa akidhibiti mikoba ya akademia ya wavulana wa klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Uingereza.
Uteuzi wake ulichochewa na ulazima wa kujazwa kwa pengo la Nick Cushing aliyeagana na Man-City mnamo Februari 2020 kwa minajili ya kuwa kocha msaidizi wa kikosi cha New York City kinachoshiriki Major League Soccer (MLS) nchini Amerika.
Alan Mahon ambaye amekuwa kaimu kocha wa Man-City, atasalia kambini mwa kikosi hicho akiwa sasa msaidizi wa Taylor.
Akizungumza pindi baada ya kurasimisha uteuzi wake, Taylor alisema kwamba yuko tayari kuzichangamkia changamoto mpya atakazokabiliana nazo huku akimakinikia zaidi majukumu yaliyopo mbele yake.
Mkuu wa masuala ya soka ya wanawake kambini mwa Man-City, Gavin Makel alisema: “Kwa kipindi cha miaka michache iliyopita, nimebahatika sana kufahamu ukubwa wa kipaji cha Gareth katika kuwakuza wanasoka na uongozi bora ambao utavunia kikosi chetu matokeo ya kuridhisha.”
Katika enzi zake za usogora, Taylor alifunga jumla ya mabao 10 kutokana na mechi 55 alizowachezea Man-City kwa kipindi cha miaka mitatu kabla ya kuwajibikia pia klabu za Crystal Palace, Sheffield United, Burnley na Nottingham Forest.
Chini ya kipindi cha miaka sita cha ukufunzi wa Cushing, Man-City walijinyanyulia jumla ya mataji sita ya haiba yakiwemo mawili ya Kombe la FA na Women’s Super League mnamo 2016.
Kwa wakati fulani, nafasi ya Cushing iliwahi kutwaliwa na Mahon kwa muda mfupi. Chini ya ukufunzi wa Mahon, Man-City waliwapepeta Bristol City 1-0 kisha kuambulia sare ya 3-3 dhidi ya Chelsea kabla ya Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza kuahirishwa kwa muda kutokana na virusi vya corona mnamo Machi 2020.
Hadi wakati wa kusimamishwa kwa ligi hiyo, Man-City walikuwa wakiselela kileleni mwa jedwali kwa alama moja zaidi kuliko Chelsea katika nafasi ya pili.