Manchester United hawajui kati ya Arsenal na Chelsea waunge gani
KUCHANGANYIKIWA ndio hali ya sasa kwa mashabiki wa Manchester United wakati Arsenal inajiandaa kulimana na Chelsea mnamo Jumanne (leo) usiku katika mtanange wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).
Mechi ya Arsenal dhidi ya Chelsea itachezewa ugani Emirates kuanzia saa nne usiku refa wa katikati akiwa ni Simon Hooper na wa mitandaoni (VAR) akiwa ni Peter Bankes.
Katika mechi tano za hivi karibuni kati ya Arsenal na Chelsea, Arsenal imeponyoka na ushindi mara tatu, ikapata sare moja na kupoteza moja.
Mashabiki sugu wa Arsenal na Man U huwa na ule uhasama wa jadi kiasi kwamba hakuna yule huitakia timu ya mwenzake ushindi katika kila mechi. Huu uhasama huwa ni wa ushemeji tu ambapo wao hupenda kutaniana.
“Ni katika hali hiyo ambapo Arsenal iliyoko juu ya jedwali kwa pointi 74 inawasinya mashabiki wa Man U ambao wengi hapa nchini Kenya wangetaka tuteremke, hata ikiwezekana, hadi katika nafasi ya mwisho ambayo ni ya 20,” asema Seneta Maalum, Karen Nyamu.
Hata hivyo, katika mechi ya usiku, mashabiki wa Man U wako kwa njia panda kuhusu washabikie klabu gani.
“Timu nne za kwanza almaarufu ‘top four’ hucheza katika Dimba la Klabu Bingwa Ulaya, yaani Champions League huku zile zinazomaliza katika nafasi ya tano hadi saba zikishiriki madimba mawili ya Europa,” asema Bi Nyamu.
Huku Man United kwa sasa ikiwa katika nafasi ya sita katika jedwali pointi zake zikiwa ni 50, Chelsea ni ya tisa ikiwa na pointi 47 lakini ikiwa na mtanange huu wa Arsenal ambapo ikipata ushindi, basi itakuwa na pointi sawa na za hao mashetani wekundu.
Vilevile, Man U inawindwa na timu ya West Ham United ambayo iko katika nafasi ya nane ikiwa na pointi 48 lakini ikiwa imecheza mechi 34 ambazo ni mbili Zaidi ya 32 za Man U kufikia sasa.
Ikiwa Arsenal itaishinda Chelsea, basi itapaa hadi pointi 77 na kuzidi kuongoza ligi hiyo.
“Hapo ndipo hesabu zetu zimetufikisha ambapo ni lazima tuingie katika nafasi saba za kwanza…Tayari, nafasi tatu za kwanza zimetuponyoka kwa kuwa hata tushinde mechi zetu zote zilisosalia na wengine juu yetu washindwe zao zote, tutamaliza tukiwa na pointi 68… Hadi sasa timu ya tatu kwa ligi ni Man City na iko na pointi 73 ikiwa na mechi sita kibindoni za kusaka pointi 18,” akasema shabiki sugu wa Man U mjini Murang’a, James Kagondu.
Kagondu alisema kwamba wana mwanya pia wa kucheza ligi ya Europa iwapo watashinda kombe la FA na ambapo kwa sasa “tumetinga awamu fainali baada ya kutandika Coventry katika nusu-fainali kupitia penalti baada ya sare ya 3-3 mnamo Jumapili”.
Hata hivyo, Kagondu alisema mkondo huo wa FA sio wa uhakika kwa kuwa mahasimu mbele yao ni Man City ambao kwa siku za hivi karibuni wamekuwa wakinyuka wapinzani bila huruma.
“Hapa kuna shida kubwa kwa kuwa mapambano ni kumaliza ligi katika nafasi bora zaidi kwa kuwa tukizubaa hata tunaweza tukamaliza katika nafasi ya 16,” akasema.
Ni katika hali hiyo ambapo mashabiki wa Man U wamegeukia maombi ya ama mechi hiyo ya Arsenal na Chelsea iishie sare na ikiwa ni lazima kuwe na mshindi, basi “Mungu amteue amtakaye”.
“Sisi hatuna nguvu kabisa kwa kuwa Arsenal kwa mara nyingine tena wametuzidi ujanja msimu huu. Tunawaombea tu washuke katika jedwali hadi nafasi ya chini zaidi iwezekanavyo ikiwa ni ya sita kwa mujibu wa hesabu,” akasema shabiki huyo kimzaha.
Timu ambazo kwa sasa ziko katika kinyang’anyiro cha mduara wa nne-bora ni Arsenal, Liverpool, Man City, Aston Villa na Tottenham Hotspur. Wanaomenyania kucheza ligi za Europa ni Aston Villa na Tottenham ambazo mmoja huenda aingie katika nafasi nne bora, Newcastle, Man United, West Ham, Chelsea, Brighton, Wolves, Fulham, Bournemouth, Crystal Palace, na Brentford.