Manchester United ingali na matumaini
KOCHA wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer amesema watajilaumu wenyewe kwa kushindwa na Wolveshampton kwa mabao 2-1 mnamo Jumanne usiku kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).
United walichukua uongozi kupitia kwa Scott McTominay kabla ya Diogo Jota kuwasawazishia wenyeji.
Beki Chris Smalling alijifunga mwenyewe na kuipa Wolves bao la ushindi baada ya beki mwenza Ashley Young kutimuliwa uwanjani kwa kupokezwa kadi nyekundu.
Baada ya kichapo hicho, Solskajaer amesema nafuu pekee kwa timu yake ni kushinda mechi tano kati ya sita zilizosalia ili kumaliza ndani ya klabu nne bora.
Hata hivyo, Ole Gunnar alisikitikia timu yake kukosa kutumia nafasi nyingi za wazi kufunga mabao, hali ambayo ingewapa ushindi na kutoa upinzani mkali kwa timu zinazowania nafasi nne za kwanza huku EPL ikielekea ukingoni.
“Tungetumia nafasi zetu vizuri tungeimarisha nafasi yetu ya kutinga nne bora. Tulikuwa tunahitaji alama 18 baada ya mechi za kimataifa kukamilika katika mechi nane zilizosalia. Tulipata alama tatu dhidi ya Watford na sasa tunahitaji alama nyingine 15 ili tusiwe na mwanya mkubwa wa kupoteza mechi nyingi na kukosa kutimiza lengo letu,” akasema Ole Gunnar.
Hii ilikuwa mara ya pili kwa United kushindwa na Wolves katika muda usiozidi wiki tatu, baada ya kichapo cha awali cha 2-1 katika pambano la FA Cup.
Labda ipo namna nzuri zaidi
Kocha huyo alipoulizwa iwapo mambo yameanza kumharibikia baada ya mfululizo wa matokeo mema, alijibu kwamba mambo hayaangaliwi kwa namna hiyo, kwa sababu mtu hawezi akaamua matokeo.
“Tunachoweza kudhibiti tu ni mtindo wa kucheza uwanjani, na tulicheza vizuri.”
Young tayari alikuwa ameonyeshwa kadi ya njano baada ya kumchezea visivyo Jota, lakini baadaye akafuatisha kwa kumchezea ngware mshambuliaji huyo matata wa Wolves.
“Mara tu unapolishwa kadi ya njano, sharti ujihadhari zaidi. Kwa kweli ulikuwa uamuzi mbaya wa Young, lakini katika hali kama hiyo, pengine alifikiria angeufikia mpira kwanza. Bila shaka angetusaidia sana kama hangetolewa,” alisema Solskjaer.
Matokeo hayo yanaiacha Manchester United katika nafasi ya tano jedwalini lakini ikiwa imecheza mechi moja zaidi ya wapinzani wao wanaowania kumaliza katika nafasi nne za kwanza.
“Nimesema tunahitaji pointi 15 katika mechi sita zilizobakia, hivyo hatupaswi kupoteza mechi yoyote,” alisema Solskjaer.