• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 5:55 AM
Manchester United katika hatari ya kuaga kipute cha UEFA baada ya kupigwa 3-1 na PSG ugani Old Trafford

Manchester United katika hatari ya kuaga kipute cha UEFA baada ya kupigwa 3-1 na PSG ugani Old Trafford

Na MASHIRIKA

MATUMAINI ya Manchester United kufuzu kwa hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) sasa ni finyu baada ya mabao mawili kutoka kwa fowadi Neymar Jr kusaidia Paris Saint-Germain (PSG) kusajili ushindi wa 3-1 mnamo Disemba 2, 2020 uwanjani Old Trafford.

Neymar aliwafungulia PSG ukurasa wa mabao katika dakika ya sita kabla ya Marcus Rashford kusawazisha mambo kunako dakika ya 32 alipofunga bao lake la tatu katika mechi nne dhidi ya miamba hao wa soka ya Ufaransa.

Hata hivyo, Marcos Marquinhos Correa aliwaweka PSG uongozini kwa mara nyingine katika dakika ya 69 sekunde chache kabla ya kiungo Fred Rodrigues wa Man-United kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kumchezea visivyo Ander Herrera aliyeingia uwanjani katika kipindi cha pili.

Bao la pili lililofungwa na Neymar dhidi ya wenyeji wao Man-United lilikuwa lake la 38 katika kivumbi cha UEFA.

Matokeo ya mechi hiyo yanasaza Man-United wakijivunia alama tisa katika Kundi H sawa na PSG na RB Leipzig waliowapepeta Istanbul Basaksehir 4-3 nchini Uturuki.

Sare ya aina yoyote kwa Man-United katika mchuano ujao dhidi ya Leipzig nchini Ujerumani mnamo Disemba 8, 2020 itawapa tiketi ya hatua ya 16-bora kwenye UEFA msimu huu.

Kabla ya kuongoza vijana wake kuvaana na Man-United, kocha Thomas Tuchel wa PSG aliungama kuwa Rashford ni msumbufu na akawataka mabeki wake kumbana kabisa.

Hii ni baada ya chipukizi huyo raia wa Uingereza kufunga penalti ya dakika za mwisho iliyowabandua PSG kwenye hatua ya mwondoano mnamo 2018-19 jijini Paris licha ya kwamba miamba hao wa Ufaransa walishuka dimbani wakijivunia ushindi wa 2-0 kutokana na mchuano wa mkondo wa kwanza uwanjani Old Trafford.

Rashford alifunga tena bao jingine la dakika za mwisho katika ushindi wa 2-1 uliosajiliwa na Man-United dhidi ya PSG katika mechi ya mkondo wa kwanza msimu huu jijini Paris, Ufaransa.

Akipania kuendeleza ubabe wake dhidi ya PSG, Rashford alishirikiana vilivyo na chipukizi Anthony Martial na wakamtatiza pakubwa kipa Kaylor Navas wa PSG.

Bao la Rashford lilikuwa lake la sita hadi kufikia sasa kwenye kampeni za UEFA na idadi hiyo ya mabao inamweka katika orodha ya wafungaji bora wa kivumbi hicho hadi kufikia sasa. Erling Haaland wa Borusia Dortmund, Alvaro Morata wa Juventus na Romelu Lukaku wa Inter Milan wanajivunia pia mabao sita kila mmoja katika UEFA msimu huu wa 2020-21.

Mabao 38 ambayo Neymar amefunga hadi kufikia sasa kwenye UEFA sasa yanamsaza na magoli mawili zaidi kumfikia Sergio Aguero wa Manchester City ambaye mchezaji wa pili baada ya Lionel Messi wa Barcelona na Argentina anayejivunia idadi kubwa zaidi ya mabao katika soka ya UEFA.

Kocha Ole Gunnar Solskjaer wa Man-United alisema ndiye anayestahili kulaumiwa kwa kutomwondoa Fred uwanjani mwishoni mwa kipindi cha kwanza ikizingatiwa kwamba alikuwa ameonyeshwa kadi ya manjano hapo awali kwa kosa la kumchezea visivyo Leandro Paredes kabla ya Rashford kusawazisha.

Man-United kwa sasa wanajiandaa kuvaana na West Hamu United mnamo Disemba 5, 2020 uwanjani London Stadium. Mchuano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na mashabiki 2,000.

Baada ya hapo, Solskjaer ataongoza vijana wake kutua Ujerumani kuvaana na Leipzig waliopigwa na Man-United 5-0 katika mchuano wa mkondo wa kwanza wa UEFA mnamo Oktoba 28, 2020 uwanjani Old Trafford.

  • Tags

You can share this post!

Giroud afunga mabao manne na kuongoza Chelsea kudhalilisha...

Msimamo mkali wa Sonko kulemaza shughuli jijini