• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 10:55 AM
Manchester United kumwajiri Pochettino iwapo Solskjaer atatimuliwa

Manchester United kumwajiri Pochettino iwapo Solskjaer atatimuliwa

Na MASHIRIKA

MANCHESTER United wamemzungumzia Mauricio Pochettino kuhusu uwezekano wa kuwa mkufunzi wao iwapo kocha wa sasa Ole Gunnar Solskjaer atatimuliwa.

Kwa mujibu wa magazeti mengi nchini Uingereza, maafisa wakuu wa Man-United waliandaa kikao na wawakilishi wa Pochettino mnamo Oktoba 5, 2020 ili kubaini iwapo atakuwa radhi kudhibiti mikoba ya kikosi hicho ambacho kimeanza vibaya kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu.

Muda wa Solskjaer uwanjani Old Trafford unaonekana kuwa mfupi baada ya vijana wake kupokezwa kichapo cha 6-1 kutoka kwa Tottenham Hotspur mnamo Oktoba 4, 2020 ugani Old Trafford.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa Man-United kupokezwa kichapo kinono katika mechi ya EPL nyumbani tangu wapokezwe kichapo kingine cha 6-1 kutoka kwa Manchester City mnamo Oktoba 2011.

Kichapo hicho kilikuwa kinono zaidi kwa Man-United kuwahi kupata tangu kocha Solskjaer apokezwe mikoba ya ukufunzi mnamo Disemba 2018 na kikubwa zaidi kwa kikosi hicho tangu Ed Woodward aaminiwe kuwa Naibu Mwenyekiti Mkuu mnamo 2013.

Matokeo hayo yalisaza Man-United katika nafasi ya 16 jedwalini mbele ya West Bromwich Albion, Burnley, Sheffield United na Fulham wanaokokota nanga mkiani. Ni West Brom pekee ndio wamefungwa idadi kubwa zaidi ya mabao (13) kuliko Man-United, Fulham na Liverpool ambao kwa sasa wamefungwa magoli 11 kila mmoja.

Ingawa Woodward hayuko radhi kumtimua Solskjaer baada ya kipute cha EPL kurejelewa mwishoni mwa mechi za kimataifa zitakazopigwa kuanzia wikendi ijayo, ni matarajio ya kinara huyo kwamba matokeo ya Man-United yataimarika.

Hata hivyo, huenda Solskjaer ambaye ni raia wa Norway akafurushwa ugani Old Trafford iwapo Man-United wataendelea kusuasua kufikia Novemba 2020.

Woodward amekuwa akivutiwa na mbinu za ukufunzi wa Pochettino aliyetimuliwa na Tottenham mnamo Novemba 2019, miezi mitano baada ya kuwaongoza kutinga fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Pochettino, 48, ametupilia mbali ofa kadhaa za kazi tangu wakati huo, zikiwemo fursa mbili za kudhibiti mikoba ya Barcelona baada ya miamba hao wa soka ya Uhispania kuwapiga kalamu wakufunzi Ernesto Valverde mnamo Januari 2020 na Quique Setien mnamo Agosti 2020.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Star nchini Uingereza, Pochettino amekuwa akisubiri fursa ya kudhibiti mikoba ya kikosi cha Man-United kwa sababu hilo ndilo kubwa zaidi katika matamanio yake.

Woodward alimtimua kocha David Moyes baada ya miezi 10 pekee ya kuhudumu kwake uwanjani Old Trafford. Kuondoka kwa Moyes kulimpisha Mholanzi Louis van Gaal ambaye pia alipigwa kalamu baada ya misimu miwili na nafasi yake kutwaliwa na Jose Mourinho aliyefurushwa mnamo Disemba 2018.

  • Tags

You can share this post!

Fulham wajinasia huduma za wanasoka watatu katika siku ya...

Kiungo Michael Cuisance atua Marseille baada ya uhamisho...