Manchester United wafukuzia kisasi dhidi ya Brighton ligini
MANCHESTER United watawania ushindi wa tatu mfululizo wa Ligi Kuu wanapolenga kulipiza kisasi dhidi ya Brighton ugani Old Trafford hapo Oktoba 25, 2025.
Ni mara ya kwanza kukutana tangu Januari ambapo Brighton waliwashangaza United 3-1.
Brighton wamelemea mashetani wekundu wa United mara sita kati ya saba wamekutana ligini ikiwemo tatu mfululizo ugani humo.
Ingawa msimu wa United haujakuwa mzuri sana chini ya kocha Ruben Amorim, ushindi dhidi ya Sunderland (2-0) na Liverpool (2-1) umeleta matumaini mapya.
Ushindi dhidi ya mabingwa watetezi Liverpool (wa kwanza uwanjani Anfield tangu 2016) ulichukuliwa kama ishara ya mabadiliko, huku mmiliki Sir Jim Ratcliffe akimpa Amorim miaka mitatu kujenga upya kikosi.
United sasa wako nafasi ya tisa, pointi tatu tu nyuma ya Manchester City wanaokamata nafasi ya pili.
Mabingwa hao wa zamani wamerejea katika hali nzuri wakiwa nyumbani wakitawala michuano yao mitatu ya mwisho Old Trafford dhidi ya Sunderland, Chelsea na Burnley.
Hata hivyo, Brighton wamekuwa mwiba kwao, wakiwafunga mara sita kwenye mechi saba za mwisho za ligi.
Lisandro Martinez bado ni majeruhi, lakini Leny Yoro anaweza kurejea katika kikosi cha United. Kuna maamuzi ya kufanywa kuhusu iwapo Amad Diallo na Diogo Dalot waendelee kama beki wa pembeni kushoto au Patrick Dorgu arejee.
Mvamizi Benjamin Sesko anaweza kuanza mbele akishirikiana na Matheus Cunha na Bryan Mbeumo, ambaye amehusika moja kwa moja katika kuzalishwa kwa mabao sita dhidi ya Brighton.
Brighton bado watakuwa bila Solly March, Adam Webster na Jack Hinshelwood. Kaoru Mitoma, Joel Veltman, Diego Gomez na Brajan Gruda watapimwa dakika za mwisho.
Ferdi Kadioglu na Maxim De Cuyper wanawania nafasi ya beki wa kushoto, huku mshambulizi stadi wa zamani wa Arsenal na United, Danny Welbeck akiwa anaongoza utafutaji wa mabao ya Brighton.
Mechi inatarajiwa kuwa ya wazi na yenye mabao, lakini United wataingia
wakiwa na kujiamini na motisha juu.