Manchester United wapata timu mteremko droo ya Uropa
Na MASHIRIKA
NYON, Uswisi
MANCHESTER United itapepetana na wanyonge LASK Linz ya Austria, katika mkondo wa 16-bora wa Ligi ya Uropa.
Katika droo iliyofanywa Ijumaa, Wolves italimana na wakali Olympiacos mnamo Machi 12.
Mechi hizo zitakuwa za kutafuta tiketi ya kuingia robo-fainali ya Uropa, ambayo ni kipute ‘toto’ cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).
United ilijinasia fursa ya kushiriki droo ya jana baada ya kulipua Club Brugge 5-0 katika mechi ya marudiano ya raundi ya 32-bora uwanjani Old Trafford, Alhamisi usiku.
Brugge walimaliza mechi wakiwa wachezaji 10 baada ya Simon Deli kuonyeshwa kadi nyekundu dakika ya 22.
Vijana wa kocha Ole Gunnar Solskjaer walikuwa wametoka 1-1 na Miamba hao wa Ubelgiji katika mkondo wa kwanza.
Lakini Man-United waliwazamisha wapinzani hao kupitia mabao ya Fred (mawili), Bruno Fernandes (penalti), Odion Ighalo na Scott McTominay.
Katika mechi hiyo nyingine Alhamisi usiku, Wolves ilisonga mbele kwa jumla ya mabao 6-3 licha ya kulemewa 3-2 na Espanyol katika mechi ya marudiano nchini Uhispania.
Droo kamili ya 16-bora ni kama ifuatavyo: Istanbul Basaksehir (Uturuki) na Copenhagen (Denmark), Olympiacos (Ugiriki) na Wolves (Uingereza), Rangers (Scotland) na Bayer Leverkusen (Ujerumani), Wolfsburg (Ujerumani) na Shakhtar Donetsk (Ukraine), Inter Milan (Italia) na Getafe (Uhispania), Sevilla (Uhispania) na Roma (Italia), Eintracht Frankfurt (Ujerumani)/Salzburg (Austria) na Basel (Uswisi), LASK Linz (Austria) na Manchester United (Uingereza).