• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Manchester United wavunja benki na kusajili beki matata Maguire

Manchester United wavunja benki na kusajili beki matata Maguire

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, UINGEREZA

MANCHESTER United wameafikiana na Leicester City kuhusu usajili wa beki matata mzawa wa Uingereza, Harry Maguire ambaye kwa sasa atatua uwanjani Old Trafford katika uhamisho utakaogharimu kiasi cha Sh10 bilioni.

Kulingana na gazeti la SunSport, Man-United watawalipa Leicester mwanzo Sh7.8 bilioni kabla ya ziada ya Sh2.2 bilioni kukamilishwa mwishoni mwa Agosti 2019.

Kusajiliwa huku kwa Maguire mwenye umri wa miaka 26 kunamfanya sasa kuwa beki ghali zaidi duniani baada ya fedha zilizowekwa mezani na Man-United kupiku kiwango cha Sh9.7 bilioni kilichotumiwa na Liverpool kujinasia huduma za Virgil van Dijk, 28, kutoka Southampton mnamo 2018.

Katika jitihada za kulijaza pengo la Maguire uwanjani King Power, Leicester tayati wameanza mazungumzo na Brighton kwa minajili ya kufanikisha uhamisho wa nyota Lewis Dunk, 27. Brighton almaarufu ‘The Foxes’ wamefichua kwamba thamani ya difenda huyo mzawa wa Uingereza kwa sasa inafikia kima cha Sh5.8 bilioni.

Awali, Maguire alihusishwa pakubwa na uwezekano wa kutua uwanjani Etihad kuvalia jezi za Manchester City waliokuwa radhi kumpokeza mshahara wa hadi Sh28 milioni kwa mwezi.

Ingawa hivyo, ofa ya Sh9 bilioni iliyotolewa na kikosi hicho cha mkufunzi Pep Guardiola kwa minajili ya maarifa ya Maguire ilikataliwa na Leicester ambao chini ya kocha Claudio Ranieri, walitawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo 2015-16.

Kusajiliwa kwa Maguire kunarasimishwa siku chache baada ya difenda huyo kuwasilisha ombi la kutaka kuachiliwa na Leicester ajiunge na kikosi chochote kingine. Kiini cha barua hiyo ya Maguire ni kusitasita kwa Leicester kuanzisha rasmi mazungumzo na Man-City na Man-United kuhusu uhamisho wake.

Kabla ya kutimuliwa kwa Jose Mourinho, kocha huyo mzawa wa Ureno alikuwa kipenzi kikubwa cha Maguire. Hata hivyo, juhudi zake za kujinasia ubunifu wa beki huyo ziliambulia patupu baada ya Man-United kukataa kufungua mifereji yao ya fedha kwa minajili ya usajili wowote katika msimu wa 2017-18.

Maguire aliwagharimu ‘Foxes’ Sh2.2 bilioni alipojiunga nao kutoka Hull City mnamo 2017 na amejitokeza kuwa tegemeo wao.

Man-City walipania kumfanya beki huyu kuwa kizibo kamili cha aliyekuwa nahodha wao, Vincent Kompany ambaye alibanduka uwnajani Etihad mwishoni mwa msimu jana na kurejea Anderlecht, Ubelgiji.

Alichokitarajia kocha

Matumaini ya Guardiola yalikuwa kwamba Maguire awe akishirikiana vilivyo na Aymeric Laporte katika safu ya nyuma ya Man-City ambao wanapania kutia kapuni ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa mara ya tatu mfululizo msimu ujao.

Mashabiki wa Leicester walishindwa kabisa kudhibiti hasira wakati klabu zilipoanza kuwasilisha ofa za kuwania huduma za masogora wao wa haiba kama vile Jamie Vardy, N’Golo Kante na Riyad Mahrez baada ya mafanikio yao ya 2015.

  • Tags

You can share this post!

PATASHIKA: Desert Foxes na Teranga Lions kukwaana kwenye...

SIHA: Unywaji holela wa pombe unasababisha madhara...

adminleo