Michezo

Manchester United yajinasia beki Telles kutoka Porto pamoja na chipukizi wawili katika siku ya mwisho ya uhamisho

October 6th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

MANCHESTER United wamemsajili beki wa kushoto, Alex Telles, kutoka FC Porto ya Ureno.

Miamba hao wa soka ya Uingereza pia wamethibitisha kwamba fowadi Amad Diallo ataingia katika sajili yao rasmi mnamo Januari 2021.

Telles ametia saini mkataba wa miaka minne uwanjani Old Trafford na atakuwa huru kurefusha kipindi cha kuhudumu kwake kambini mwa Man-United kwa mwaka mmoja zaidi.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 27 ambaye amechezea Ureno mara moja pekee, alifanikisha uhamisho wake hadi Man-United kwa kima cha Sh1.9 bilioni. Anajivunia kufungia Porto jumla ya mabao 21 kutokana na mechi 127 katika mashindano yote.

Man-United pia waliweka mezani kima cha Sh1.2 bilioni kwa minajili ya fowadi Facundo Pellistri, 18, aliyejiunga nao kutoka kambini mwa Penarol nchini Uruguay kwa mkataba wa mieka mitano.

Man-United wamerasimisha uhamisho wa chipukizi, Diallo, 18, kwa kima cha Sh2.6 bilioni.

Usimamizi wa Man-United umekuwa ukimfuatilia Diallo kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita nchini Italia.

Kinda huyo raia wa Ivory Coast alifungia Atalanta bao katika mchuano wake wa kwanza katika Ligi Kuu ya Italia (Serie A) mnamo Oktoba 2019.

Hadi kufikia sasa, Diallo hajawajibishwa na Atalanta ya kocha Gian Piero Gasperini msimu huu wa 2019-20. Sogora huyo aliweka historia kwa kuwa mwanasoka wa pili aliyezaliwa katika mwaka wa 2002 baada ya Ansu Fati wa Barcelona kuwahi kufunga bao katika mojawapo ya Ligi Kuu za bara Ulaya; yaani EPL (Uingereza), Ligue 1 (Ufaransa), Bundesliga (Ujerumani), Serie A (Italia) na La Liga (Uhispania).

Man-United wamekuwa wakifuatilia pia maendeleo ya Pellistri, 18, kwa mwaka mmoja uliopita tangu kipaji chake kitambuliwe na mvamizi wa zamani wa Man-United na aliyekuwa kocha wa Penarol, Diego Forlan.