Michezo

Manyatta United, Kitale Queens zabeba Chapa Dimba

June 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na JOHN KIMWERE

KWA mara nyingine wawakilishi wa Nairobi walishindwa maarifa na wapinzani wao katika fainali za kitaifa za ubingwa wa Chapa Dimba na Safaricom Season Two 2018/2019 kwa upande wa jinsia ya kiume na kike.

Manyatta United (Mkoa wa Nyanza) na Kitale Queens (Mkoa wa Bonde la Ufa) zilitawazwa washindi wapya baada ya kutesa katika fainali zilizosakatiwa uwanjani Kinoru Stadium, mjini Meru.

Baada ya mafanikio hayo, timu hizo kila moja ilipongezwa kwa kitita cha Sh1 milioni na wadhamini wa kipute hicho; kampuni ya Safaricom.

Manyatta United iliipepeta Al-Ahly ya Bonde la Ufa mabao 2-1 katika fainali.

Nao warembo wa Acakoro Ladies kutoka Nairobi walimaliza mbili bora baada ya kunyoroshwa kwa magoli 4-2 na Kitale Queens kupitia penalti baada ya kutoka nguvu sawa mabao 2-2 katika muda wa kawaida.

Millicent Ayuwa wa Kitale Queens (kulia) akabiliana na Sylvia Makungu wa Acakoro Ladies katika fainali ya kitaifa ya Chapa Dimba na Safaricom Season Two, uwanjani Kinoru Stadium, Meru. Kitale Queens ilishinda kwa mabao 4-2 kupitia penalti baada ya sare ya mabao 2-2 katika muda wa kawaida. Picha/ John Kimwere

Manyatta United iliyopigiwa chapuo kubeba taji hilo ilipata ushindi huo baada ya Mark Ochieng na Benson Ochieng kila mmoja kuitingia bao moja. ”Licha ya wapinzani wetu kuteremsha upinzani wa kufa mtu tuna furaha tele hatimaye tumetwaa ubingwa wa kitaifa mwaka huu,” golikipa wa Manyatta United, Nicholas Munangwe alisema.

Kwenye nusu fainali Manyatta United iliikanyaga Lugari Blue Saints (kutoka eneo la Magharibi) mabao 2-1 nayo Al-Ahly kupitia mipigo ya matuta ilivuna mabao 3-2 mbele ya South B United (Nairobi).

Nayo Kitale Queens ilitafuna Barcelona Ladies kwa mabao 6-0 wakati Changamwe Ladies (Pwani) ikilala kwa mabao 4-2 mbele ya Acakoro Ladies.

Kwa tuzo za binafsi tuzo ya mchezaji anayeimarika (MVP) iliwaendelea Abdurahman Adullahi wavulana (Ah-Ahly) na Daisy Busia kitengo cha wasichana wa Kitale Queens.

Kitengo cha wavulana, Dennis Atsenga (Lugari Blue Saints), Mark Ochieng na Benson Ochieng wote (Manyatta) walituzwa wafungaji bora huku Jane Njeri wa Barcelona Ladies akibeba tuzo hiyo kwa wasichana. Nao Nicholas Munangwe (Manyatta United) na Phyllis Chemutai (Kitale Queens) waliibuka magolikipa bora kwa wavulana na wasichana mtawalia.