Maombi ya Arsenal kwa Spurs yakosa kujibiwa
USHINDI wa Manchester City dhidi ya Tottenham Hotspur umeiweka Arsenal katika mazingara magumu ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu baada ya kusubiri kwa kipindi cha miaka 20.
Huku kila timu ikibakisha mechi moja kumaliza msimu, kutokana na ushinsi huo wa mabao 2-0 Jumanne usiku ugani Tottenham Hotspur, Man City wako kileleni baada ya kukusanya pointi 88, pointi mbili zaidi ya Arsenal.
Ushindi katika mechi yao ya mwisho dhidi ya West Ham utawezesha vigogo hao wa soka nchini hapa kutwaa ubingwa huo kwa mara ya nne mfululizo.
Arsenal walikuwa wakiomba majirani zao Spurs wawafanyie msaada kwa kuchapa City ili waendelee kubakia katika kinyang’anyiro cha kutwaa ubingwa wa taji hilo baada ya kusubiri tangu msimu wa 2003/2004.
Lakini mashabiki wa Arsenal walishangaa kuona Spurs wakichezacheza bila jitihada zozote za kuwania ushindi, hasa katika kipindi cha pili baada ya Erling Haaland kufunga mabao hayo dakika za 51 na 91 mtawalia.
Spurs chini ya kocha Ange Postecoglou walipoteza nafasi nyingi katika mechi hiyo iliyoshuhudiwa na zaidi ya mashabiki 60,000.
“Kutokana na matokeo hayo, hatuwezi kuipuiku Aston Villa katika nafasi ya nne, lakini lazima tushinde Sheffield Jumapili katika mechi ya mwisho ili tumalize katika nafasi ya tano na kufuzu kwa michuano ya Europa League, msimu ujao,” alisema Postecoglou.
Ilikuwa mechi ngumu, lakini hatukutumia vyema nafasi tulizopata, hasa katika kipindi cha kwanza. Tuliwasumbua katika sehemu ambazo wamezoea kutamba. Tutajilaumu wenyewe. Tulifungwa bao la kwanza kwa sababu tulifanya makosa ya kijinga,” aliongeza raia huyo wa Australia mwenye umri wa miaka 58.
“Tulitaka Spurs ifungwe au itoke sare, lakini tumeshuhudia kinyume na tulivyotarajia, sasa tunasubiri tena kuona kama West Ham itawachapa katika mechi ya mwisho,” alisema shabiki sugu wa Arsenal, Benard Wanyonyi akiwa Nairobi.
Licha ya kushindwa katika mechi hiyo, mashabiki wa Spurs walionekana kufurahia matokeo hayo kutokana na uhasama wao wa jadi dhidi ya Arsenal. Spurs na Arsenal zimekuwa mahasimu wakuu.
Katika mechi hiyo, kipa Stefan Ortega aliyeingia katika nafasi ya Ederson aliyeumia na kutolewa, alionyesha kiwango kizuri kwa kuokoa makombora kadhaa kutoka kwa washambuliaji wa Spurs karibu na eneo la hatari.
Wakati Manchester City wakimaliza msimu uwanjani mwao Etihad, Arsenal watakuwa Emirates kukaribisha Everton, lakini tayari dalili za ubingwa wa taji kwenda Etihad zimeanza kuonekana baada ya City kulaza Spurs.