Marefa wa mechi kati ya Kariobangi Sharks na Asante Kotoko watajwa
Na GEOFFREY ANENE
REFA Ghislain Atcho kutoka Gabon ameteuliwa kusimamia mechi ya Kombe la Mashirikisho (Confederation Cup) kati ya wenyeji Kariobangi Sharks na wageni Asante Kotoko itakayosakatwa katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani jijini Nairobi hapo Desemba 15, 2018.
Katika mechi hii ya mkondo wa kwanza ya raundi ya kwanza, Atcho atakuwa refa wa kupuliza kipenga. Atasaidiwa na wanyanyuaji vibendera Theophile Vinga na Angelo Malekou Mambana pia kutoka Gabon.
Vilevile, Afisa wa nne Isidore Carlos Nze anatoka Gabon. Kamishna wa mechi ni Maxwell Mtonga kutoka Malawi naye Songuifolo Yeo kutoka Ivory Coast atakuwa afisa wa kuangalia kazi ambayo marefa hao watafanya.
Sharks na Kotoko zinakutana kwa mara ya kwanza katika historia yao. Sharks, ambayo pia inashiriki mashindano yoyote ya Bara Afrika kwa mara yake ya kwanza kabisa, ilitinga raundi ya kwanza baada ya kubandua nje Arta Solar7 kutoka Djibouti kwa jumla ya mabao 9-1 baada ya mikondo miwili.
Kotoko ilipata tiketi ya bwerere baada ya Cameroon kuchelewa kuwasilisha jina la timu iliyofaa kukutana na Waghana hawa. Timu hizi zitarudiana mjini Kumasi mnamo Desemba 22, 2018.