Mariga aisaidia Mabazenga FC kunasa taji la Kriss Darling
NA JOHN KIMWERE
ALIYEKUWA mchezaji wa kimataifa MacDonald Mariga ameisaidia Mabazenga FC kutawazwa mabingwa wa mashindano ya Kriss Darling Super Cup baada ya kuinyuka Kibra United goli 1-0 katika fainali iliyoandaliwa uwanjani Woodley Kibera, Nairobi.
Mchezo huo ulishuhudia ushindani mkali huku kila upande ukishambulia ngome ya wapinzani wao kwenye juhudi za kutafuta ubingwa huo.
Hata hivyo Mabazenga FC ilianza kuwazidi ujanja wapizani wao katika kipindi cha pili kufuatia ujio wake Maringa ambaye amekuwa akishiriki soka la kulipwa nchini Italia alipokuwa akipigia klabu ya Real Oviedo.
Mchango wake uliibeba Mabazenga FC kuvuna goli la pekee lililofumwa kimiani na Musa Masika ambaye husakatia Wazito FC.
Nao wachana nyavu Abdullattif Nassur na Kelvin Senya kila mmoja alitikisa wavu mara moja na kubeba Gogo Boys kumaliza ya tatu ilipochuna mabao 2-0 mbele ya Uweza FC.
”Licha ya kutoibuka mabingwa wa kipute hicho cha makala ya tatu nawashukuru wachezaji wangu wote kwa kujitahidi na kufaulu kuibuka kati ya tatu bora msimu huu,” ofisa mkuu wa Gogo Boys, Abdull Suleiman alisema.
Kwenye nusu fainali, Gogo Boys ilikung’utwa magoli 2-1 na Mabazenga nayo Kibra United iliandikisha ushindi wa goli 1-0 mbele ya Uweza FC.
Uweza FC ya kocha, Charls Kaindi ilikuwa miongoni mwa vikosi vilivyopigiwa upatu kutwaa taji hilo. Kwenye robo fainali Olympic Talented ilizimwa na Gogo Boys, Uweza FC ilibamiza Kibra Lexus, FC Bundes FC ilizamishwa na Kibra United nayo Mabazenga FC ilisajili mabao 2-1 dhidi ya Kipaji FC.