Michezo

Masaibu ya kifedha yatawalemaza Starlets AWCON – Mwendwa

October 23rd, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

RAIS wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) Nick Mwendwa amekiri nafasi ya Harambee Starlets katika Kombe la Afrika la Wanawake (AWCON) mwaka 2018 imo hatarini kutokana na matatizo ya kifedha.

Aidha, Mwendwa, ambaye amesema Starlets inahitaji Sh43 milioni kufanikisha maandalizi na mechi mbili za kirafiki, ameshambulia Bunge kwa masaibu ya timu za taifa kuhangaika kifedha kutokana na kujikokota kwake kurasimisha Hazina ya Kitaifa ya Michezo.

Akizungumza na wanahabari jijini Nairobi, Mwendwa hasa ameimulika Kamati ya Bunge ya Majukumu Maalum, ambayo inaongozwa na Mwakilishi wa wanawake wa kaunti ya Uasin Gishu, Gladys Shollei.

Ameiomba itatue maswali iliyoibua ambayo yalifanya shughuli ya Hazina ya Kitaifa kuchapisha sheria kuhusu jinsi fedha zitatumika, kusisimashwa. “Kamati ya Shollei ilikuwa na maswali kadhaa kuhusu jinsi fedha hizi zitatumiwa. Maswali hayo bado hayajatatuliwa. Ushiriki wa Kenya katika AWCON sasa uko hatarini kwa sababu hatuna fedha.

Tuna ripoti kwamba Hazina ya Kitaifa ya Michezo ina kati ya Sh10 bilioni na Sh12 bilioni. Hata hivyo, hatuwezi kupata fedha kusaidia Harambee Starlets kwa sababu maswali hayo hayajajibiwa.

Tunaomba kamati hiyo iharakishe kutatua maswali hayo ili kuhakikisha hazina ianze kufanya kazi juma hili. Ni muhimu sana maswali hayo yatatuliwe haraka. Hazina hii ya michezo isipoanza kufanya kazi siku chache zijazo, itatubidi tuombe Wakenya fedha ili tuweze kupeleka Starlets nchini Ghana kwa mashindano hayo.

Wapinzani wa Kenya katika Kundi B, ambao ni Super Falcons ya Nigeria, Banyana Banyana ya Afrika Kusini na Shepolopolo ya Zambia, walitaja vikosi vyao Oktoba 19 na hata kuanza mazoezi.

Kenya bado haijafanya hivyo. FKF imesema Jumatano kwamba kocha David Ouma atatangaza kikosi chake baadaye Oktoba 23. Kulingana na Mwendwa, Starlets itaanza mazoezi Oktoba 29.

Ratiba ya AWCON 2018 (Saa za Kenya):

Novemba 17

Ghana na Algeria (Accra Stadium, 6.30pm, Kundi A)

Mali na Cameroon (Accra Stadium, 9.30pm, Kundi A)

Novemba 18

Nigeria na Afrika Kusini (Cape Coast Stadium, 6.30pm, Kundi B)

Zambia na Kenya (Cape Coast Stadium, 9.30pm, Kundi B)

Novemba 20

Ghana na Mali (Accra Stadium, 6.30pm, Kundi A)

Cameroon na Algeria (Accra Stadium, 9.30pm, Kundi A)

Novemba 21

Nigeria na Zambia (Cape Coast Stadium, 6.30pm, Kundi B)

Kenya na Afrika Kusini (Cape Coast Stadium, 9.30pm, Kundi B)

Novemba 23

Cameroon na Ghana (Accra Stadium, 7.00pm, Kundi A)

Algeria na Mali (Accra Stadium, 7.00pm, Kundi A)

Novemba 24

Kenya na Nigeria (Cape Coast Stadium, 7.00pm, Kundi B)

Afrika Kusini na Zambia (Cape Coast Stadium, 7.00pm, Kundi B)

Novemba 27

Namba 1 Kundi A na Namba 2 Kundi B (Accra Stadium, 6.30pm, nusu-fainali)

Namba 1 Kundi B na Namba 2 Kundi A (Cape Coast Stadium, 9.30pm, nusu-fainali)

Novemba 30

Mechi ya kutafuta nambari tatu (Cape Coast Stadium, 7.00pm)

Desemba 1

Fainali (Accra Stadium, 7.00pm)