• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 11:29 AM
Mashabiki 5,000 kuhudhuria marudiano ya Comoros na Kenya katika gozi la kufuzu kwa AFCON 2021

Mashabiki 5,000 kuhudhuria marudiano ya Comoros na Kenya katika gozi la kufuzu kwa AFCON 2021

Na CHRIS ADUNGO

COMOROS wamefichua kwamba wataruhusu mashabiki 5,000 kuhudhuria mchuano wa kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Afrika (AFCON) dhidi ya Harambee Stars ya Kenya mnamo Novemba 15, 2020.

Mchuano huo utapigiwa katika uwanja wa Stade de Maulozini jijini Moroni siku nne baada ya Kenya kuwa wenyeji wa Comoros kwenye mchuano wa tatu wa Kundi G uwanjani Nyayo, Nairobi.

Habari za mashabiki kuruhusiwa ugani kuwatilia shime wanasoka wa Comoros dhidi ya Kenya zimethibitishwa na kocha Amerine Abdou ambaye pia amefichua kikosi atakachokitegemea katika mechi mbili zijazo dhidi ya Stars.

“Tofauti na mechi ya mkondo wa kwanza itakayosakatiwa ndani ya uwanja mtupu, mechi yetu ya marudiano dhidi ya Kenya itatandiwa mbele ya mashabiki 5,000 jijini Moroni,” akasema Abdou.

Kocha Jacob ‘Ghost’ Mulee wa Stars ni mwingi wa matumaini kwamba kikosi chake kitafanya vyema katika mkondo wa kwanza jijini Nairobi licha ya kutokuwepo uwanjani.

“Tungefurahua sana kuwa mashabiki ugani – watushangilie na kushereheka kila bao ambalo tutafunga dhidi ya Comoros. Lakini itakuwa salama zaidi iwapo watasalia nyumbani na kufuatilia baadhi ya matukio runingani,” akasema Mulee.

“Itatulazima kuchuma nafuu zaidi kutokana na mechi ya nyumbani hata bila mashabiki. Matumaini yangu ni kwamba tutashinda nyumbani na hata ugenini. Naaminishwa zaidi na kiwango cha kuimarika kwa kikosi baada ya vipindi vichache vilivyopita vya mazoezi,” akasema Mulee kwa kufichua kwamba motisha na ushindani zaidi unatarajiwa kambini baada ya wanasoka wa ughaibuni kuwasili wote kufikia Novemba 9, 2020.

Abdou ambaye alipokezwa mikoba ya Comoros mnamo 2014, amefichua kikosi cha wanasoka 23 atakaotegemea dhidi ya Stars. Fowadi Ben Al Fardou, 31, wa Red Star Belgrade nchini Serbia ni miongoni mwa wachezaji hao.

Comoros kwa sasa wanaongoza Kundi G kwa alama nne baada ya kusajili ushindi wa 1-0 dhidi ya Togo na kuambulia sare tasa dhidi ya Misri katika mechi mbili za ufunguzi. Stars walianza kampeni zao za kufuzu kwa fainali zijazo za AFCON dhidi ya Misri kwa sare ya 1-1 mnamo Novemba 14, 2019 ugenini kabla ya kusajili matokeo sawa na hayo dhidi ya Togo mnamo Novemba 18, 2019 jijini Nairobi.

KIKOSI CHA COMOROS:

MAKIPA: Salim Ben Boina (FC Martigues), Ali Ahamada (SK Brann).

MABEKI: Kassim Abdallah (Athletico Marseille), Abdallah Ahmed Mohammed (SV Zulte Waregem), Chaker Alhadhur (Chateaurox), Ahmed Soilihi (Quievily Rouen), Nadjim Abdou (FC Martigues), Kassim Mdahoma (Lyon SC), Bendjaloud Youssouf (Le Mans).

VIUNGO: Youssuf Mchangama (EA Guigamp), Rafidine Abdullah (Stade Lausanne Ouchy), Ibrahim Madi (Martigues), Yacine Bourhane (Niort), Nasser Chamad (Gaz Metan), Mohamed Youssef (AC Ajaccio), Said Bakari (RKC Waalwjik).

MAFOWADI: Faiz Selemani (KV Courtrai), Ibroihim Youssuf (Club Volcano), Nakibou Aboubakari (Stade Briochin), Ali Mmadi (Tours FC), Ahmed Mogni (FC Annecy), Faiz Mattoir (AC Ajaccio), El Fardou Ben Mohamed (Red Star Belgrade).

  • Tags

You can share this post!

Southampton raha tele baada ya kuongoza jedwali la EPL kwa...

Mabao ya Fernandes na Cavani yapunguza joto na presha...