• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Mashabiki wa Arsenal: Bora tu tumalize EPL juu ya Man U tuko sawa

Mashabiki wa Arsenal: Bora tu tumalize EPL juu ya Man U tuko sawa

Na MWANGI MUIRURI

MASHABIKI wa timu ya Arsenal sasa wanadai kwamba bora tu wamemaliza wakiwa juu ya Manchester United katika jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), taji linaweza kaa kando.

Hata Arsenal sasa ikose kushinda mechi zake mbili iliyosalia nazo nayo Man U ishinde zake zote tatu ilizo nazo, haiwezi ikaibuka bora kuliko ‘The Gunners’.

Ni katika hali hiyo ambapo mashabiki wa Arsenal wanawapa Man U almaarufu The Red Devils pole za msiba wa machozi ya mamba katika maombolezo ya kukomolewa magoli 4-0 na timu ya Crystal Palace mnamo Jumatatu usiku.

“Angalau sisi watu wa Arsenal hata tukose taji hatuna shida bora tu tumalize ligi tukiwa mbele ya Man United,” asema Askofu Yohana Gichuhi, ambaye majuzi alidai Kai Havertz ni mwokozi pale klabuni Arsenal.

Mabao ya M. Olise kunako dakika za 12 na 66, kisha la J. Mateta katika dakika ya 40 na lile la T. Mitchel katika dakika ya 55, yaliinamisha nyuso za wapenzi wa Man U katika usiku ulioishia kuwa wa giza totoro.

“Haya ni mafuriko yanayosomba Man U hadi nje ya saba-bora hivyo basi kuituma kuwa mshiriki wa kawaida wa msimu wa 2024/25 nje ya madimba ya Europa na Klabu Bingwa Ulaya (Uefa),” akafoka shabiki wa Chelsea Bw John Mwangi katika mtandao wake wa WhatsApp.

Aliendelea na utani wake ambapo aliiweka picha ya nyani wa Man U Andre Onana akiwa kama malaika wa kunyoosha mikono kubariki mashuti yakiingia nyavuni badala ya kuyanyaka.

Naye Seneta Karen Nyamu aliambia Taifa Spoti mnamo Jumanne kwamba “tumeshuhudia jinsi ambavyo Man U wako katika hali mbaya kiufundi huku wakitungoja mnamo Mei 12, 2024, ambapo tuko na mechi na wao”.

“Ikiwa hii ndio Man U tutakayokutana nayo, nawasihi tu watafute kijisababu cha kukosa kushiriki mtanange huo,” Bi Nyamu alikejeli.

Hata hivyo, wafuasi wa Man U wamekaa ngangari wakidai kwamba “sisi hushinda tukitaka na kupoteza kwa hiari…hakuna cha mkosi kwetu, yote hufanyika kwa utaratibu”.

Shabiki Isaac Wairimu alisema kwamba masimango hayo ni kelele bila maana.

“Kelele tunazopigiwa eti mara hatutashiriki dimba la Europa… mara sijui Arsenal itatunyuka… ziite kelele za chura,” akasema Bw Wairimu.

Alisema kwamba “sisi tutacheza Europa kupitia kuibuka mabingwa wa FA na pia tuwapige Arsenal ugani kwetu Old Trafford…afadhali tutolewe kwa uwanja tukiwa tumezirai kwa kujituma tukihangaisha Arsenal”.

Bw Wairimu alisema “heri sisi tunafunga msimu bila aibu ya kuwekwa matumaini feki kwamba tuna uwezo wa kuchukua taji la EPL msimu huu kama walivyofanyiwa wenzetu wa Arsenal ambao kombe watakaloinua ni la masikitiko”.

  • Tags

You can share this post!

Wabunge kuamua hatima ya Linturi mnamo Mei 13

Wanaume wanyemelea wajane kwa kisingizio cha kujikinga mvua

T L