Michezo

Mashabiki wa Gor wampokea Oliech kwa shangwe

January 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

Mfungaji bora wa timu ya taifa ya Kenya, Dennis Oliech alikaribishwa kwa shangwe na mashabiki katika mechi yake ya kwanza alipoingia kama mchezaji wa akiba kuchezea timu yake mpya ya Gor Mahia iliyotamatika 1-1 dhidi ya Mathare United uwanjani Kasarani, Januari 6, 2019.

Hata hivyo, baada ya mchango wake wa dakika 22 umegawanya mashabiki. Mashabiki wengi wa Gor hawajaridhishwa naye, ingawa kuna sehemu ndogo waliomiminia sifa kama Abraham Onyango, ambaye amesema, “Oliech yuko sawa.”

Naye Michael Nyapoya amewataka mashabiki wa Gor kukumbuka jagina wa Camweroon, Roger Milla aliyeng’aa katika Kombe la Dunia mwaka 1990 akiwa na umri wa miaka 42.

“Msidharau Oliech…Jagina Roger Milla alistaafu kutoka soka kabla ya kubadili mawazo na kurejea kuchezea Indomitable Lions akiwa na umri wa miaka 42 na alicheza soka safi katika Kombe la Dunia mwaka 1990 akifunga mabao matamu…Oliech bado ana uwezo wa kutandaza soka kwa hivyo tafadhali mpeni nafasi.”

Baadhi ya mashabiki waliokuwa na hisia kali kuhusu mshambuliaji huyu mwenye umri wa miaka 33 ni Kijana Wa Mum. Hakuficha kero lake akisema, “Nimeudhika sana na Oliech.” Naye Bensouda Muzungu aliuliza, “Mnapochezesha mshambuliaji mwenye umri mkubwa kabisa Oliech mnatarajia nini?”

George Ramji hakuelewa sababu iliyofanya Gor ilisajili Oliech. “Oliech, mlinunua kwa nini?” Naye Calvin Pongo anasema Gor ilipoteza fedha kwa kununua mchezaji huyu wa zamani wa Mathare United (Kenya), Al Arabi (Qatar), FC Nantes, AJ Auxerre na AC Ajaccio (Ufaransa) na Dubai CSC (Milki za Kirabu). “Hapo kwa Oliech, K’Ogalo ina fedha nyingi za kuharibu.” Aliikeli Gor kwa kusajili Oliech “kutoka kwa makavazi.”

Oliech alistaafu Julai 1 mwaka 2015 kabla ya kutua Gor siku chache zilizopita kwa kandarasi ya miaka miwili, huku ripoti zikisema atakula mshahara mkubwa kuliko wachezaji wenzake kwenye Ligi Kuu wa Sh350, 000.