Michezo

Mashabiki wa Ingwe waombwa kutokata tamaa ligini

February 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA CECIL ODONGO

MASHABIKI wa AFC Leopards wameombwa kutokata tamaa na badala yake waendelee kuishabikia timu hiyo inayokalia nafasi hatari ya kushushwa ngazi kwenye ligi.

Katibu Mkuu wa AFC Leopards Oscar Igaida amewataka mashabiki hao kukoma kuelekezea uongozi lawama kutokana na matokeo mabaya Ingwe imekuwa ikisajili lakini wafike uwanjani kwa wingi ili kuwapa motisha wachezaji katika mechi kali dhidi ya Ulinzi Stars wikendi hii na Mathare United wiki ijayo.

“Kwa kweli ni wakati kila mdau kambini mwa chui anafaa kutekeleza wajibu wake kuhakikisha timu inajikwamua na kusalia ligini. Tuna kocha mpya ambaye tuna imani atatambisha Ingwe hadi turejee kwenye nafasi za timu nane bora kabla mkondo wa kwanza wa KPL uliosalia na mechi tano haujatamatika,” akasema Bw Igaida wakati wa mahojiano na Taifa Leo Dijitali..

Afisa huyo vile vile alisisitiza kwamba malalamishi yote yaliyoibuliwa na wachezaji yametatuliwa na yanayosalia ni kupokea ripoti ya kocha mwishoni wa msimu ili klabu ifanye usajili wa wachezaji wa haiba watakaovumisha Ingwe msimu ujao.

“Ni vizuri niseme kwamba masuala yote yanayohusu maslahi ya wachezaji yametatuliwa. Maamuzi yote kuhusu usajili mwishoni mwa msimu tumemwaachia kocha ambaye tayari ameleta mabadiliko makubwa na kuzidisha motisha kwa wachezaji kwenye kambi zetu za mazoezi,” akatanguliza

“Hata hivyo tutalenga sana kuwasajili wanasoka kwenye safu za ushambulizi na kiungo ambazo tumeona ni dhaifu. Kuvuja kwa safu hizo kumechangia matokeo haya ikizingatiwa kwamba Marvin Omondi, Ezekiel Seda na Said Tsuma bado wanauguza jeraha,” akaendelea Igaida.

Wakati uo huo Igaida aliambia Taifa Leo Dijitali kwamba watazindua rasmi mdhamini mpya wa timu hiyo ambayo ni kampuni ya Umbro mwishoni wa mwezi huu.

Umbro ilitia saini mkataba wa kudhamini Ingwe kwa muda wa miaka mitatu mwezi uliopita na itakuwa na jukumu la kutoa jezi yenye nembo yake kwa wachezaji na pia kuziuza kwa mashabiki.

Igaida na maafisa wa Ingwe wiki jana waliunda kamati ya kuokoa Ingwe kwa jina ‘AFC Rescue Team’ itakayoshirikiana na Kamati Kuu ya Klabu (NEC) kutafuta namna ya kupata utatuzi wa masuala yanayochangia matokeo duni msimu huu.